Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
Benki ya Biashara na Maendeleo ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (Trade and Development Bank-TDB), itaikopesha Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wenye thamani ya dola za Marekani milioni 400, sawa na takriban shilingi bilioni 900, kwa ajili ya ujenzi wa Reli ya Kiwango cha Kimataifa (SGR) na Mradi wa kuzalisha umeme wa gesi wa Kilwa.
Hayo yamesemwa Jijini Dar es Salaam na Rais wa Benki hiyo yenye Makao yake Makuu Jijini Nairobi Nchini Kenya, Bw. Admassu Tadesse, alipokutana na kufanya mazungunzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani.
Bw. Tadesse amesema kuwa Benki yake imetenga kiasi cha dola za Marekani milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kati ya kisasa pamoja na kiasi kingine kama hicho kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa gesi wa Kilwa mkoani Lindi.
“Tanzania ni mdau mkubwa wa Benki hii ikiwa inashika nafasi ya 7 kati ya nchi na taasisi 37 zinazomiliki hisa zake ambapo inamiliki hisa asilimia 6.4” alisema Bw. Tadesse.
Bw. Admassu Adesse amesema kuwa hadi machi mwaka 2018, benki yake inatekeleza miradi 11 ya maendeleo nchini Tanzania, katika sekta ya kilimobiashara, huduma za benki na fedha, nishati, ukuzaji miundombinu na viwanda, yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani 284.6 milioni.
“Tuna miradi mingine iliyoidhinishwa na Benki, inayokadiriwa kufikia dola za Marekani milioni 157 na kiasi kingine cha dola za Marekani milioni 660 ambacho kimepangwa kutolewa kwa Tanzania ili kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta za kilimobiashara, ujenzi, kemikali na petroli pamoja na sekta ya nishati” aliongeza Bw. Adesse.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango ameipongeza benki hiyo kwa kuendelea kujiimarisha kimtaji na kiuendeshaji na kwamba Tanzania inapokea kwa mikono miwili ahadi ya Benki hiyo ya kushiriki katika ujenzi wa miradi ya kipaumbele ya Taifa ikiwemo ujenzi wa Reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (SGR) na Mradi wa kuzalisha umeme wa Kilwa, itakayochochea uchumi wa nchi.
Aliahidi kuwa atahakikisha mazungumzo kuhusu upatikanaji wa mkopo huo nafuu yanakamilika ndani ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia sasa ili fedha hizo ziweze kupatikana.
Kwa upande wake Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, alisema kuwa mradi wa kuzalisha umeme wa gesi wa Kilwa, utakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 318 na utaongeza kiwango cha upatikanaji umeme nchini ambacho hivi sasa kimefikia megawati 1500.
“Lakini pia tuna vijiji 176 vinahitaji umeme ambapo kati yake vijiji 120 viko kwenye visiwa na vinahitaji kupatiwa huduma ya nishati ya umeme na TDB imekubali kusaidia ujenzi wa miradi ya umeme kwa kutumia nguvu ya maji ambapo kila mradi utazalisha megawati 10 za umeme” alisema Dkt. Kalemani
TDB inaundwa na nchi 22 za kiafrika, nchi mbili ambazo si nchi za kiafrika pamoja na taasisi za uwekezaji 13 na kufanya idadi ya nchi na taasisi ambazo ni wana hisa, zinazounda benki hiyo, kufikia 37.
Post A Comment: