Tanzania na Zambia zimekubaliana kutumia kituo kimoja cha forodha kilichojengwa mjini Tunduma.
Lengo na ushirikiano huo ni kupunguza na kudhibiti msongamano wa magari na uingizwaji wa mizigo kwa njia za magendo.
Makubaliano hayo yamefanyika jana Ijumaa Julai 20, 2018 baina ya naibu kamishna wa forodha wa mamlaka ya mapato Tanzania (TRA), Qamdiyay Akonaay na kamishina wa forodha wa mamlaka ya mapato Zambia (ZRA), Sydney Chibbabbuka baada ya kukagua miundombinu ya majengo katika mpaka wa Tunduma na Nakonde.
Akizungumzia na waandishi wa habari mjini Tunduma, Akonaay amesema wamefikia makubaliano hayo kwa lengo la kupunguza msongano wa magari na usimamizi wa usafirishaji wa mizigo ili kuongeza mapato na kuthibiti njia za magendo za kupitisha bidhaa katika mipaka ya nchi hizo.
"Kituo cha pamoja cha forodha kitaanza kufanya kazi Julai 26 mwaka huu. Wafanyakazi wa ZRA na TRA watafanya kazi katika ofisi moja. Ushirikiano huu utakuwa chachu ya kukuza uchumi wa mapato hususani kwa upande wa Tanzania," amesema.
Naye Chibbabbuka amesema ushirikiano huo utakuwa na faida nyingi katika usafirishaji wa mizigo na kupunguza msongamano uliokuwepo.
Amesema nchini Zamziba tayari wamepata eneo la maegesho ya magari kutoka Tanzania, wanatarajia kuanza ujenzi wa uzio katika eneo hilo mwakani.
Post A Comment: