Msanii Steve Nyerere, amesema siyo kweli kuwa amepewa fedha na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) ili aweze kuwashawishi wasanii wenzake juu ya mabadiliko mapya ya tozo yaliyotangazwa na baraza hilo siku za hivi karibuni ili wakubaliana nayo.

Steve amebainisha hayo leo Julai 13, 2018 baada ya wadau mbalimbali wa filamu na muziki kumshambulia kupitia ukurasa wake wa kijamii kuwa amepatiwa fedha 'fungu lake' ndio maana anajifanya kutaka kukaa kikao na wasanii wenzake ili wapate ufumbuzi juu ya jambo hilo ambalo limekuwa gumzo kwa sasa.

"BASATA haiwezi kunipa fedha 'fungu' lolote kwa ajili yangu mimi huko ni kuichafua, mimi ni nina nguvu gani mpaka wanilipe. Lazima niwe upande wa wenzangu ambao ni wasanii na msema ukweli siku zote ni mpenzi wa Mungu, kiukweli milioni tano kwa msanii ni pesa nyingi sana hata ingekuwa milioni moja bado shida ingekuwepo", amesema Steve

Pamoja na hayo, Steve ameendelea kwa kusema "kama kweli BASATA walitaka kutusaidia walipaswa waanze kutupa kazi wao kwa kututengenezea mifereji ya kupata matangazo ili ndio watake hizo pesa walizozitaka. Kwa namna moja ama nyingine hayo makampuni yakikataa kutupa matangazo sisi na yakaenda kuwapa raia wa kawaida hao BASATA watakuwa wanapata nini zaidi ya hasara tu. Duniani kote msanii anapata fedha kupitia matangazo".

Mbali na hilo, Steve Nyerere ameitaka jamii kutoliingiza suala hilo katika mlango wa kisiasa licha ya kuwa yeye yupo ndani ya chama cha Mapinduzi (CCM).

Siku za hivi karibuni Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) liliweza kufanya mabadiliko mbalimbali katika tozo zao za utoaji wa huduma ikiwemo ya makampuni kulipa milioni tano kwa BASATA endapo watamtumia msanii kufanya tangazo la aina yoyote, jambo ambalo limekuwa likipingwa na wasanii wengi nchini wakidai kuwa kwa kitendo hicho watakosa kazi.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: