Na Lorietha Laurence-WHUSM,Manyara.
Serikali imendelea kuweka msukumo wa kukuza Sekta ya filamu nchini,kwa kuendeleza utafiti, ubunifu na teknolojia ikiwemo kujenga mazingira wezeshi kwa wadau wake ili kuleta matokea chanya katika tasnia hiyo .
Hayo yamesemwa jana Mkoani Manyara na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe alipokuwa akifungua mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo wadau wa filamu katika Mkoa huo yaliyoandaliwa na Bodi ya Filamu nchini.
Dkt. Mwakyembe ameeleza kuwa Mkoa wa Manyara una mazingira mazuri yenye fursa ya kuandaa filamu nzuri zenye ubora na uhalisia wa vivutio mbalimbali vinavyopatikana katika Mkoa huo.
“Watu wa Manyara tumieni fursa hii nzuri mliyoipata katika mafunzo haya ambayo yanatolewa bure kwa kutengeneza filamu nzuri, ukizingatia mazingira yenu yana uhalisia mzuri wa kuvutia” amesema Dkt, Mwakyembe.
Aidha alizidi kufafanua kuwa kuna mambo mengi ya kuweka katika filamu, ikiwemo tamaduni zinazopatikana katika Mkoa wa Manyara, milima pamoja na uoto wa asili kitu kitakacholeta hali ya utofauti na wa kipekee .
Naye Kaimu Katibu Tawala kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara Bw. Misaile Musa alizidi kuwasisitiza washiriki wa mafunzo hayo kujifunza kwa makini ili kuleta mabadiliko kwa kutengeneza filamu bora zenye viwango.
Kwa Upande wake Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu nchini. Bibi. Joyce Fissoo amesema lengo la mafunzo hayo ni kuleta mabadiliko katika tasnia ya filamu nchini, ili kuwa na waandaji bora wa filamu.
Post A Comment: