Jeshi la Polisi mkoani hapa kupitia Kamanda wake wa mkoa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng’anzi, limetaja mambo matano ambayo yakifanyika basi kutakuwa na mafanikio zaidi katika kuushinda uhalifu.
Akizungumza katika mahojiano yaliyofanywa na Redio Sunrise ya Jijini hapa kupitia kipindi chake cha “Kwa ajili ya Nchi yako” kinachorushwa hewani kila siku ya Ijumaa kuanzia saa 9:00 Alasiri hadi saa 10:00, Kamanda Ng’anzi alisema, kwanza kabisa kila mwananchi anatakiwa ajue ana wajibu wa kutoa taarifa za matukio ya Uhalifu na Wahalifu zinatokea katika eneo lake.
Pili alisema ni lazima askari wa Jeshi hilo watoe huduma bora na kwa kiwango cha juu kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuwasikiliza pindi wanapoeleza shida zao lakini pia kwenda haraka katika maeneo yaliyoripotiwa kutokea uhalifu.
Tatu alisema lazima kila askari adumishe na kuongeza kiwango cha nidhamu hali ambayo itasaidia baadhi ya wanaokwenda kinyume kutofanya kazi kwa mazoea na hivyo watafanya kazi kwa kufuata taratibu zilizopo.
Nne alisema askari watatakiwa kufanya kazi kwa kuheshimu Utu pamoja na kufuata Maadili ya kazi yao na tano kufanya kazi kwa Uweledi na Usasa ambapo askari atafanya kwa namna alivyofunzwa lakini pia kuendana na kasi ya ukuaji wa Teknolojia na mwisho wa siku waone kwa jinsi gani wananchi mkoani hapa wanaridhishwa na utendaji wa Jeshi hilo
Post A Comment: