Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti (kulia) akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha Mati Super Brands Ltd, David Mulokozi (kushoto) wakati akikagua vinjwaji vinavyotengenezwa na kampuni hiyo, katikati ni mbunge wa Jimbo la Babati Mjini Pauline Gekul na Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji huo Mohamed Kibiki.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Pastory Mnyeti (watatu kulia) akiongoza ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo mjini Babati, kulia ni mbunge wa viti maalum wa mkoa huo Ester Mahawe.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti, akizungumza na wananchi wa mjini Babati ambapo alisikiliza kero zao na kuwapa majawabu, kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Babati Mohamed Kibiki na mbunge wa Jimbo la Babati Mjini Pauline Gekul.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Alexander Mnyeti amemshukia vikali mbunge wa Jimbo la Babati Mjini, Pauline Gekul (Chadema) kutodandia maendeleo yanayofanywa na Serikali ikiwemo ujenzi wa barabara na kuwadanganya wananchi kuwa yamesababishwa na Chadema.
RC Mnyeti aliyasema hayo jana mjini Babati kwenye mkutano wa hadhara baada ya Gekul kujinasibu kuwa maendeleo yanayoonekana Babati yanafanywa na Chadema.Mkuu huyo wa mkoa aliwaeleza wananchi kuwa fedha za bajeti ya mkoa wa Manyara alienda mwenyewe bungeni jijini Dodoma kuzitetea lakini Gekul na wapinzani walipinga ila wabunge wa CCM walitetea.
"Acheni kudandia maendeleo ya watu. Diwani au mbunge atapata wapi fedha za kukamilisha miradi ya maendeleo kwenye halmashauri ambayo haina vyanzo vya mapato vya uhakika kama serikali kuu isipotoa fedha zake na kukamilisha hayo," alisema Mnyeti.
Alimtaka mbunge huyo kuungana na wapenda maendeleo wa kweli na kuachana na siasa za kudanganya wananchi ili hali bungeni wanapinga maendeleo kwa kukataa bajeti.
Alisema baada ya serikali kujenga kilomita 4.5 za barabara za lami ndani ya mji wa Babati hivi sasa kutaongezwa kilomita nyingine 10 za lami ili kufanikisha miundominu bora ya eneo hilo ambalo ni makao makuu ya mkoa huo.
"Hizo barabara zilizotengenezwa mjini Babati na zinazoendelea kujengwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais John Magufuli alizoahidi wakati wa kampeni na siyo vinginevyo wapinzani msidandie maendeleo," alisema Mnyeti.
Alisema kila kiongozi anapaswa kubeba mzigo wake mwenyewe kwa kufanya mikutano mwenyewe na siyo kusubiri kudandia ziara ya mkuu wa mkoa na kuongopea wananchi waliojitokeza kwa wingi.
Awali, Mhe. Gekul ambaye alikuwa kwenye msafara wa RC Mnyeti alipopewa nafasi ya kuwasalimia wananchi alisema Chadema imefanikisha maendeleo mengi Babati tangu wachaguliwe mwaka 2015.
"Tangu wananchi walipotuchagua na kutupa nafasi ya kuongoza halmashauri ya mji wa Babati tumefanikisha miradi mbalimbali ikiwemo sekta ya afya, elimu, maji na barabara na tutaendelea kuwatumikia," alisema Gekul.
Post A Comment: