Rais Dkt. John Magufuli
Salamu hizo za Dkt. Magufuli amezitoa leo Julai 30, 2018 na kusema kwamba anamkumbuka Sheikh Fereji kwa ucha Mungu wake, ukarimu, upendo kwa wananchi na namna alivyokuwa akiunga mkono juhudi za kudumisha amani na kusukuma mbele maendeleo.
"Nimesikitishwa sana na kifo cha Sheikh Fereji, nilipokuwa nikienda Mwanza alikuwa miongoni mwa viongozi wa dini waliokuja kunipokea na amekuwa akifanya kazi ya Mwenyezi Mungu kwa mapenzi makubwa na nchi yake, pole sana Mufti wa Tanzania na nakuomba unifikishie salamu zangu za pole kwa familia yake, Waislamu wote wa Mkoa wa Mwanza na nchi nzima pamoja na wote walioguswa na msiba huu", amesema Rais Magufuli.
Sheikh Salum Hassani Fereji alifariki usiku wa kuamkia Julai 28, 2018 katika hospitali ya Rufaa ya Bugando Mkoani Mwanza alipokuwa amelazwa kwa matibabu ya ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu.
Maiti ya Sheikh Salum Hassani Fereji ilisaliwa Julai 29, 2018 katika msikiti wa Raudhwa uliopo mtaa wa Lumumba jijini Mwanza na kuzikwa siku hiyo hiyo ambapo viongozi wa dini akiwamo Mufti wa Tanzania Aboubakary Zubeir walihudhuria katika mazishi hayo pamoja na viongozi wa serikali.
Post A Comment: