Mbunge wa Jimbo la Mwanga Jumanne Maghembe amesema kuwa atagombea kiti hicho mwaka 2020 na kukanusha uvumi wa baadhi ya watu wanaodai kuwa anamuandaa mwanae Ngwaru Maghembe ambaye ni Mbunge wa Binge la Afrika Mashariki kuchukua nafasi hiyo.
Maghembe aliyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ndorwe alipotembelea ujenzi wa barabara ya Lembeni, Kilomeni, Ndorwe inayojengwa kwa kiwango cha changarawe yenye urefu wa kilomita 30 pamoja na kusikiliza kero za wananchi.
Aidha Maghembe alisema kuwa hana mpango wa kuacha siasa na kumwachia mwanae Kama baadhi ya watu wanavyozusha kwani bado ana nguvu za kuwatumikia wananchi kupitia nafasi hiyo ya Ubunge.
"Bado nina nguvu na ari ya kuwatumikia wananchi kazi hii ninaimudu vyema hivyo nitagombea tena kuhusu suala la Ubunge wa Mtoto wangu alichaguliwa na Bunge la Tanzania kuiwakilisha nchi katika Bunge la Afrika Mashariki" Alisema Maghembe
Pia amemshukuru Raisi Dk.John Pombe Magufuli kwa kuifanya barabara hiyo kuwa barabara ya taifa na kuiweka chini ya Tanroad jambo ambalo litasidia barabara hiyo ipitike na kupunguza adha kwa wananchi.
Alisema kuwa barabara hiyo Kwa sasa inajengwa kwa kiwango cha changarawe ili iweze kupitika na iwapo fedha zaidi zitapatikana barabara hiyo itaboreshwa kwa kiwango cha Lami.
Mbunge huyo amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa wakandarasi ili kukamilisha ukarabati wa barabara hiyo muhimu itakayorahisisha mawasiliano na biashara miongoni mwa vijiji vilivyopo katika wilaya hiyo
Post A Comment: