Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetangaza tarehe rasmi ya uchaguzi mdogo wa Ubunge katika jimbo la Buyungu pamoja na udiwani katika kata 79 za Tanzania Bara ambapo siku ya uchaguzi huo imepangwa kuwa Agosti 12 mwaka huu.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage wakati alipokuwa akizungumza katika mkutano na wajumbe wa tume hiyo mbele ya waandishi wa habari leo Julai 10, 2018 na kusema kwamba wamefikia maamuzi hayo baada ya tume hiyo kupokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai kuhusiana na uwazi wa jimbo hilo.
"Tumeshaandaa ratiba ya uchaguzi huu, tunatarajia fomu zianze kuchukuliwa Julai 8 hadi 14, uteuzi wa wagombea utafanyika Julai 14. Kampeni tunatarajia zianze kufanyika kuanzia Julai 15 hadi Agosti 11 na uchaguzi utakuwa Agosti 12", amesema Jaji Kaijage.
Pamoja na hayo, Jaji Kaijage ameendelea kwa kusema "uchaguzi huu mdogo wa Ubunge na Udiwani utahusisha jimbo la Buyungu, halmashauri ya Kakonko mkoani Kigoma na Udiwani katika kata 79 zilizopo katika halmashauri 43 kwenye mikoa 24 ya Tanzania Bara. Katika uchaguzi huu vituo vya kupigia kura vitakuwa vile vile vilivyotumika katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015".
Jimbo la Buyungu limekuwa wazi kutokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Kasuku Samson Bilago aliyefariki Mei 26 mwaka huu na kupelekea jimbo hilo kuwa wazi hadi sasa.
Post A Comment: