Naibu waziri wa elimu sayansi na Teknolojia Mheshimiwa William Olenasha Ameagiza kukamatwa kwa mwalimu wa Shule ya Sekondari Loliondo Erick Kalaliche kwa kosa la kumbaka mwanafunzi wake wa kidato cha tatu (jina limehifadhiwa) ambaye kwasasa amehamia mkoa wa Lindi baada ya Kutenda Kosa Hilo.
Akizungumza katika kikao cha dharura kilichofanyika katika makao makuu ya halmashauri ya Ngorongoro Mheshimiwa Olenasha amesema kwamba jambo hilo linasikitisha na kuidhalilisha sekta ya Elimu na lazima hatua za kisheria na Kinidhamu zichukuliwe mara moja.
Amesema wizara ya Elimu haiwezi kuvumilia walimu ambao wanafundisha watoto ambao pia ni kama wazazi wanaofumbia macho vitendo vya vichafu ambavyo vinarudisha nyuma sekta ya Elimu na juhudi za serikali ya kuhakikisha watoto wanapata elimu Bora.
Afisa elimu wa wilaya ya Ngorongoro Bwana Emanuel Sukums amekiri mwalimu huyo kutenda kosa la kumbaka mwanafunzi huyo ambapo kitendo hicho kilifanyika mwezi wa tatu na kujulikana mwezi wa sita ambapo hakuna hatua zozote za kinidhamu zilizochukuliwa.
Amesema kuwa mwalimu Erick alimchukua mwanafunzi huyo ambaye alikuwa anasoma kidato cha tatu katika shule hiyo ya Sekondari Loliondo na kumpeleka nyumba ya kulala wageni na kumbaka.
Tarehe 9 July 2018 naibu waziri wa Elimu sayansi na Teknolojia Mh William Olenasha alifanya ziara ya Kushtukiza shule ya sekondari Loliondo na kuhoji kuhusiana taarifa za mwalimu huyo ambapo mwalimu mkuu wa Shule hiyo Bi Neema Mchao alikosa majibu sahihi mbele ya Naibu waziri lakini baadae kukiri kwamba mwalimu alihama shuleni na alikuwa ametenda kosa hilo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Loliondo Bi Neema Mchao amekiri kufuatilia jambo hilo lakini alipohojiwa kwanini hakuchukua hatua za kinidhamu alisema yeye aliachia mamlaka husika kwasababu hata yeye jambo hilo lilimsikitisha.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye ni mkuu wa wilaya ya Ngorongoro Rashidi Mfaume Taka amesema kuwa utaratibu unafanyika kurudishwa kwa mwalimu huyo kutoka mkoa aliyohamishiwa kuja Ngorongoro kwa kuwa kitendo alichokifanya ni Udhalilishaji katika wilaya hiyo.
Kufuatia kikao hicho mkuu wa Polisi wilayani Ngorongoro amemtaka Mkuu wa Shule ya Sekondari Loliondo pamoja na Afisa Elimu kufika kituoni kwa ajili ya Uchunguzi zaidi wa tukio hilo
Post A Comment: