Na Judith Mhina-MAELEZO
Katika kuhakikisha azma ya Tanzania ya Viwanda inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt John Pombe,Ofisi ya Msajili wa Hazina imefanikiwa kufufua baadhi ya viwanda vilivyoasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mkoani Mbeya.
Juhudi za kufufua viwanda hivyo zimeonekana katika viwanda vitatu, ambavyo ni kilichokuwa kiwanda cha nguo cha Mbeya au Mbeya Textile, baadaye New Mbeya Textile na sasa East Africa Starch LTD. Kingine ni kiwanda cha Zana Za Kilimo – ZZK ambacho sasa ni Christopher Mwita Gachuma Investments LTD – CMG Investments LTD na kiwanda cha Kampuni ya Wakulima wa Chai wa Katumba na Mwakaleli.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya Bi Mariam Mtughuja amesema “Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliacha viwanda vitano vikubwa Mbeya. Ambavyo ni Kiwanda cha Nguo cha Mbeya au Mbeya Textile, Zana Za Kilimo –ZZK, kiwanda cha Wakulima wa Chai, Viwanda Vidogo Vidogo-SIDO na kiwanda cha Nyama au Tanganyika Packers Mbeya”.
Juhudi za Ofisi ya Msajili wa Hazina za kufufua viwanda vilivyokufa zimeleta faraja kubwa kwa wakazi wa mbeya, kwani watafaidika na ajira pamoja na kukuza kipato kutokana na biashara ndogondogo zitakazokuwa zikiendeshwa pembezoni mwa viwanda hivyo.
Ufufuaji wa viwanda umekumbwa na baadhi ya changamoto mkoani Mbeya ambapo eneo la viwanda Vidogo vidogo SIDO limevamiwa na wananchi na kuwa soko, na kiwanda cha Nyama bado tunamuomba Msajili wa Hazina azidi kukipigania ili kiweze kupata mwekezaji mwenye nia ya kweli maana wale wote walioonyesha nia ya kuwekeza hawakurudi. Alisema Katibu Tawala.
Sifa kubwa ya Mkoa wa Mbeya ni kubahatika kuwa na hali ya hewa nzuri ambayo inaruhusu kila aina za mazao kulimwa na kustawi,hivyo wawekezaji wanafursa ya kuwekeza katika maeneo mbalimbali ambapo mali ghafi inapatikana hapa au Mikoa ya jirani kama Katavi, Iringa, Njombe, Rukwa, Ruvuma na Songwe.
Kwa sasa Mkoa wa Mbeya uko katika maandalizi ya kufanya kongamano la Uwekezaji na biashara kuanzia tarehe 26 mpaka 27 Julai, wafanyabiashara na Wawekezaji wenye nia ya kuwekeza wanakaribishwa.
Kongamano hilo limeandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania – TANTRADE na Mgeni rasmi anatarajia kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Mkoa umetenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji hususan viwanda kulingana na Halmashauri husika,na Halmashauri 7 zimetenga viwanja kwaajili hiyo. Pia taarifa za biashara na uwekezaji zinatolewa na nyingine zitatolewa kupitia vyombo vya habari ikiwemo na mitandao ya kijamii, ili mfanya biashara au mwekezaji aamue ni sehemu gani muhimu ambayo unaweza kuwekeza au kufanya biashara. Alisema Katibu Tawala huyo wa Mkoa wa Mbeya.
Alitolea mfano kuwa Halmashauri ya Jiji la Mbeya imetenga jumla ya viwanja 52 kwenye eneo la ukubwa ekari 74,169, pia Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya imetenga jumla ya viwanja 22 katika eneo la ekari 3805 kwa ajili ya viwanda.
Halmashauri ya Rungwe imetenga ekari 32 kwa ajili ya viwanja 5 vya viwanda, Halmashauri ya Chunya imetenga viwanja 132 lenye ukubwa wa ekari 100, Busokelo viwanja 21, Halmashauri ya Mji Kyela imetenga kiwanja 1, Halmashauri ya Mbarali imetenga viwanja 15,pamoja na Halmashauri ya Rungwe yenye viwanja 5.
Hadi kufikia Februari, 2018 jumla ya viwanja vilivyotengwa kwa matumizi ya viwanda ni 251 vyenye jumla ya ukubwa wa ekari 78,150.2 kati ya lengo la kutenga viwanja 502 ifikapo Juni, 2020.
Mkoa wa Mbeya ni kati ya mikoa michache hapa Tanzania ambayo imebahatika kuwa na hali ya hewa nzuri inayokubali kustawi kwa mazao mbalimbali na yanazalishwa kwa wingi. Mfano, mahindi, viazi mviringo, viazi vitamu, ndizi za aina mbalimbali, mchele bora unaopendwa wa kienyeji, ngano na shayiri, Chai, matunda ya aina mbalimbali kama maparachichi yanayosafirishwa nje ya nchi pamoja na mboga za kila aina.
Pia kuna uzalishaji unaoridhisha wa kokoa pamoja na miti ya mikaratusi na mieresi ambayo kwa kiasi kikubwa inatumika katika kuendeshea mashine ya kuzalisha unyevunyevu unaohitajika wakati wa kuzalisha majani ya Chai katika kiwanda cha Wakulima Wadogo wa Katumba Mwakaleli na Rungwe.
Mkoa wa Mbeya pia ni mzalishaji mkubwa wa maziwa ambapo Wilaya ya Tukuyu ina idadi kubwa ya ngombe wa maziwa ikifuatiwa na Wilaya ya Chunya yenye idadi kubwa wa ngombe wa asili aina ya Zebu wenye uzalishaji mkubwa wa nyama.
Vile vile, kuna aina mbalimbali za madini kama vile dhahabu, makaa ya mawe, pamoja na vivutio mbalimbali vya watalii ambavyo vinaufanya mkoa huo kuwa sehemu muhimu kwa wawekezaji na wanaotaka kufanya biashara mbalimbali.
Post A Comment: