MGOMBEA UDIWANI KATIKA KATA YA MWAKAKATE, MJI WA TUNDUMA MKOANI SONGWE, AYUBU MLIMBA.

MGOMBEA udiwani katika Kata ya Mwakakate, Mji wa Tunduma mkoani Songwe, Ayubu Mlimba, amenusurika kifo baada ya nyumba yake kuchomwa moto na watu wasiojulikana siku moja kabla ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi huo.

Mlimba ni miongoni mwa madiwani watano waliokihama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Februari 6 na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza na Nipashe nyumbani kwake jana, Mlimba alisema tukio hilo lilitokea majira ya 6.30 usiku wa kuamkia jana akiwa amelala na mkewe.

Akisimulia mkasa huo, Mlimba alisema kuwa akiwa amelala, alishangaa kuona kitu alichodhani ni maji kikimiminwa kupitia dirisha la chumba alichokuwa amelala na dakika chache alisikia mlio mithili ya bomu ukisikika ndani ya chumba chao na moto kuwaka.

Aliendelea kueleza kuwa katika jitihada za kujiokoa na kuokoa mali zilizokuwapo ndani, walimwaga maji na kuita majirani, lakini wakati wa harakati za uokoaji zikiendelea, alikanyaga mafuta ya moto yaliyokuwa yamesambaa chumbani na kuungua miguu yake yote.

Mlimba alisema walitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi na usiku huo huo askari wake walifika eneo la tukio na kuanza kuchunguza chanzo cha tukio hilo.

Alidai kuwa polisi walikuta madumu ya lita tano, yote yakiwa na mafuta ya dizeli yaliyochanganywa na petroli pamoja na nondo chini ya dirisha.

Mlimba alisema analihusisha tukio hilo na masuala ya kisiasa kutokana na baaadhi ya viashiria ambavyo amewahi kukumbana navyo.

“Niliwahi kufyekewa mahindi shambani ekari mbili, kuwekewa maiti nje ya nyumba yangu na leo wamechoma nyumba yangu,” alisema Mlimba.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Mathias Nyange, alipotafutwa na Nipashe jana kuzungumzia tukio hilo, alisema hawezi kulitolea ufafauzi hadi aonane na mwandishi ana kwa ana siku ya kazi.

Nipashe pia ilizungumza na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Momba, Twaha Maulid, ambaye alisema kitendo kilichofanywa dhidi ya mgombea wao huyo huenda kikawa kisasi kutokana na kukihama chama chake cha zamani.

Alisema katika uchaguzi wa marudio wa madiwani unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao, wamewateua wagombea wote watano ambao walitoka Chadema kupeperusha bendera ya CCM.

Alisema chama (CCM) kinalaani tukio hilo, lakini akasisitiza wanasubiri kukamilika kwa upelelezi wa Jeshi la Polisi ndipo watoe tamko rasmi.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: