Mfumuko wa bei kwa Juni 2018 umepungua hadi asilimia 3.4 ikilinganishwa na asilimia 3.6 ya Mei mwaka huu.
Mkurugenzi wa sensa ya watu na takwimu za jamii, Ephraim Kwesigabo amesema hali hiyo imechangiwa na kupungua kwa bei za bidhaa zisizo za vyakula.
Akizungumza leo Jumatatu Julai 9, 2018 amesema bidhaa zisizo za chakula zimechangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa mfumuko wa bei kati ya Juni 2017 na Juni 2018.
"Bia zilipungua kwa asilimia 1.1, gharama za ukarabati wa vifaa vya umeme na viyoyozi kwa asilimia 1.8, gesi ya kupikia kwa asilimia 5.6 na majiko ya mkaa kwa asilimia 2.0," alisema Kwesigabo.
Kuhusu mfumuko wa bei za vyakula na vinywaji baridi, alisema mpaka Juni uliongezeka hadi asilimia 3.4 kutoka asilimia 2.6 uliokuwapo Mei.
Wakati mfumuko ukipungua nchini, hali imekuwa tofauti kwa nchi za Afrika Mashariki.
Nchini Uganda, amesema kwa mwaka ulioishia Juni mfumuko umeongezeka hadi asilimia 2.2 kutoka asilimia 1.7 uliokuwapo mwaka ulioishia Mei. Hata Kenya, mfumuko huo umeongezeka hadi asilimia 4.28 kutoka asilimia 3.95 za mwaka ulioishia Mei, 2018.
Post A Comment: