Makamu Mwenyekiti wa kamati ya kuivusha Yanga, Meck Sadick, amesema hana taarifa rasmi za kujiuzulu kwa Mwenyekiti wake katika kamati hiyo Tarimba Abbas, bali amezisikia tu kama watu wengine.
Sadick ambaye ni moja ya wanachama wenye heshima ndani ya klabu hiyo, ameeleza kusikitishwa na taarifa hizo na kuahidi kumfuata Tarimba na kuongea naye binafsi ili kujua nini sababu ya yeye kukaa kando.
''Kwasasa sio wakati mzuri wa kujadili kila jambo hata kama kweli kuna wakati mgumu tunapitia, Tarimba anaweza kuwa amekasirishwa na kitu binafsi pengine nikiongea naye mimi anaweza kusema tatizo na akarudi kwenye nafasi yake ila kwasasa tusubiri kwanza'', - amesema.
Tarimba alitangaza kuachia nafasi yake jana jioni kwa kile alichoeleza kuwa ni kutokuwepo kwa maelewano kati ya viongozi wa sasa wa klabu na viongozi wa kamati maalum ya kuivusha Yanga katika kipindi cha mpito ambayo yeye alikuwa anaiongoza kama Mwenyekiti.
Meck Sadick ambaye ni mkuu wa mkoa mstaafu aliyehudumu katika mikoa ya Dar es salaam na Kilimanjaro kwa vipindi tofauti, aliteuliwa kuwa makamu mwenyekiti wa kamati hiyo kupitia mkutano mkuu wa klabu uliofanyika Mei 20 huku Tarimba Abbas yeye akiteuliwa kuwa Mwenyekiti.
Tarimba ameiongoza kamati hiyo kwa siku 50, lengo kuu ikiwa ni kusaidia timu kwenye maeneo kadhaa ikiwemo usajili na maandalizi ya uchaguzi kwaajili ya kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Mwenyekiti Yusuf Manji. Aidha kamati hiyo ilipata baraka za baraza la wadhamini la Yanga chini ya Mwenyekiti George Mkuchika ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala bora.
Post A Comment: