Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amesema hataki kuona wafungwa nchini wanaishi kama ndege wa angani.
Amesema hayo akimaanisha kuwa hawalimi ila wanakula bure, badala yake wanatakiwa wafanye kazi na kujitafutia chakula wao wenyewe badala ya kusubiri kupewa chakula na Serikali.
Lugola ameyasema hayo jana Julai 16 wakati akihojiwa katika kipindi cha Tuambie kilichorushwa na kituo cha televisheni cha TBC1 Jumatatu usiku, na kubainisha kuwa amewaagiza wasaidizi wake kupitia sheria vizuri na kumpelekea mpango mzuri wa utekelezaji wa agizo la Rais, la kuwatumia wafungwa kufanya kazi za kilimo na ufugaji na kujitafutia chakula wao wenyewe.
“Hata kama ni meno, lazima walimie meno, watatumia meno yao kulima mahindi, kulima maharage ili wajilishe, na nimemwambia Inspekta Jenerali wa Magereza, katika hili sitaki kisingizio cha aina yoyote".
Lugola amesema kuwa amemueleza Inspekta Jenerali wa Magereza kutumia Shirika la Uzalishaji Mali, Benki ya Kilimo na TIB kuchukua mikopo katika kutekeleza agizo hilo la Rais.
Waziri Lugola amesema utoaji wa chakula bure gerezani umepelekea baadhi ya wafungwa kuona gerezani kama ndiyo sehemu ya kupumzika na kula bure bila kufanya kazi, na kusababisha baadhi yao kila wanapobakisha mwezi mmoja kumaliza vifungo au wakimaliza vifungo na kuachiwa huru, wamekuwa wakifanya makosa mengine kwa makusudi ili warudi tena gerezani.
"Wanajitafutia makosa na kuendelea kukaa bure na kula chakula bure bila kufanya kazi,"amesema.
Post A Comment: