Na. Elinipa Lupembe.
Kufuatia mpango mkakati wa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli, unaolekeza elimu ya msingi kuwa ni haki ya lazima kwa kila mtoto, na kwa sasa itaanzia darasa la awali mpaka kidato cha nne, wananchi wa kijiji cha Kiseriani kata ya Mlangarini halmashauri ya Arusha, wameunga mkono mpango mkakati huo wa Serikali kwa vitendo.
Wananchi hao wameamua kujenga shule ya sekondari ambayo haijawahi kuwepo kijijini hapo, tangu enzi na enzi ili watoto wao wapate elimu hiyo ya msingi ndani ya kijiji chao na kuwaondolea watoto wao ada ya kutembea umbali mrefu kwenda kupata elimu ya sekondari.                          
Wananchi hao wa Kiseriani,  wamefikia uamuzi huo makini, mara baada ya kupokea fedha kiasi cha shilingi milioni 150, kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe kama fidia ya shamba ambalo kijiji hicho kilitoa kwa chuo hicho.      
Licha ya  wananchi hao kukabiliwa na changamoto nyingine, wameamua kutumia fedha hizo kuwekeza kwenye elimu, kwa kujenga shule mpya ya sekondari, kwa kuwa watoto katika eneo hilo hulazimika kutembea mpaka kijiji cha Mlangarini kupata elimu ya sekondari, eneo ambalo lina umbali mrefu kijiografia.                        
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Dkt. Wilson Mahera amesema kuwa, kwa mujibu wa miongozo ya serikali ya awamu ya tano,  ujenzi wa shule hiyo hautatumia wakandarasi na badala yake utatumia 'Force Account', utaratibu unaoruhusu kutumia 'local fundis' mafundi wa kijijini kwa kusimamiwa na kamati zilizochaguliwa na wananchi wa eneo hilo chini ya uangalizi wa watalamu wa halmashauri.
Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa,  tayari wananchi wa kijiji cha Kiseriani wamesha chagua Kamati ya ujenzi na Kamati ya manunuzi, zitakazohusika na usimamizi wa hatua zote za ujenzi wa miundombinu ya shule hiyo na kuongeza kuwa majengo hayo yanatakiwa kukamilika, mwishoni mwa mwaka huu 2018.
"Kazi ya kamati hizi ni kusimamia hatua zote za ujenzi huku zikisimamia manunuzi ya vifaa kuanzia mwanzo mpaka kukamilika kwa ujenzi na tunategemea ujenzi huo kukamilika mapema mwaka ili Januari wanafunzi waanze kusoma hapo" amesema Mkurugenzi huyo.  
Aidha mkurugenzi Mahera amewataka wananchi wa kijiji cha Kiseriani, kushiriki kwa hali na mali na kuhakikisha ujenzi umekamilika kulingana na thamani ya fedha zilizopo 'value for money'.                                                      
Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Kiseriani mheshimiwa Zebedayo Thomas amesema kuwa,  licha kuipongeza serikali ya awamu ya tano na Mkurugenzi wa halmashauri ya Arusha kwa kuungana nao,  kuhakikisha watoto wao wanapata elimu ya sekondari ndani ya eneo lao, amewaomba watalamu  kushirikiana nao wakati wote wa utekelezaji wa mradi huo.  
Juliana Lekeye mkazi wa Kiseriani amesema kuwa, kwa sasa watoto wa Kiseriani  wamepata neema kubwa, kutokana na ukweli kwamba, wamekuwa wakitembea umbali mrefu kwenda  shule ya Sekondari Mlangarini zaidi ya Kilomita kumi kila siku.    
"Watoto wetu wanateseka sana kutembea kwenda shule na wakati mwingine, wengine wanakata tamaa na kuamua kuacha shule kwa umbali" amesema Juliana
Kaimu Mhandisi wa Ujenzi, halmashauri ya Arusha, Mhandisi Bibie Manzi amefafanua kuwa, kiasi hicho cha fedha kitatumika kujenga vyumba sita vya madarasa na meza na viti, ofisi ya walimu na samani za ofisi pamoja na vyoo vya wanafunzi na walimu.
Ameongeza kuwa,  tayari timu ya watalamu imetembea na kukagua eneo la ujenzi na kuandaa michoro na ujenzi huo unategemea kukamilika ndani ya miezi mitano huku taratibu za  ujenzi zikitarajiwa kuanza muda mfupi kuanzia sasa.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: