Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla ametoa siku 40 kwa wakazi wa vijiji vinavyopakana na hifadhi ya pori la akiba la Kijereshi wilayani Busega Mkoa wa Simiyu, kuhama eneo hilo.

Dk Kigwangalla amemuagiza meneja wa hifadhi hiyo, Diana Chambi kuhakikisha kabla ya siku hizo kuisha, awaandikie barua wananchi hao wanaodaiwa kufanya shughuli za kijamii katika eneo hilo lenye ukubwa wa mita 500, kuhama mara moja ili ziwekwe alama za kuonyesha mwisho wa hifadhi hiyo.

Ametoa agizo hilo leo Alhamisi Julai 19, 2018 katika ziara yake ya kutembelea hifadhi hiyo, kushangazwa na idadi kubwa ya wananchi waliojenga nyumba za kudumu ndani ya hifadhi hiyo, kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji.

Amesema ikifika Agosti 31, 2018 wananchi watakaoshindwa kuondoka eneo hilo, wataondolewa kwa nguvu.

“Muda nilioutoa ukimalizika kazi inaaza mara moja, hapa hakuna utani  hii ni hifadhi lazima itunzwe na kulindwa, tukiwaacha hawa wataendelea na ujangili na kuweka mifugo,” amesema.

“Kuanzia Septemba Mosi operesheni inaanza kwa wale wote watakaogoma kuondoka.”

Katika hatua nyingine, waziri huyo ameitaka kampuni ya Kijereshi Tented Camp iliyowekeza kwenye pori hilo,  ndani ya miezi mitatu kurejesha kwa msajili wa ardhi hati ya eneo lenye ekari 1,160 lililoko ndani ya hifadhi hiyo kwa maelezo kuwa walipewa kimakosa.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: