Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amewaomba wananchi wanaozungumza kimzaha juu ya matukio ya watu kutekwa na watu wasiojulikana kutofanya hivyo.
Pia, ametoa ushauri kwa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (Tantrade) kuwa na siku maalumu ya kudumisha amani na umoja katika maonyesho inayoandaa.
Dk Bashiru alisema hayo jana alipotembelea Maonyesho ya 42 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF) yanayoendelea katika viwanja vya maonyesho vya Mwalimu J.K. Nyerere, barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Alisema jitihada zinazofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli ya kupambana na ufisadi na rushwa zinajenga vitisho jambo ambalo linawafanya watu wasioitakia mema nchi kutofurahia.
“Vitisho vingi sana duniani vya kiusalama, kuna watu nasikia wanafanya mzaha wa kiusalama, wanazungumza watu wanaopotea. Wanazungumza kimzaha, kulikuwa na matatizo pale Kibiti ukienda Rufiji (mkoani Pwani), hayajatatulika lakini tunashukuru vyombo vya ulinzi na usalama wamekabiliana nao,” alisema Dk Bashiru.
Alisema, “Kuna vitisho vingi sana, bahati mbaya kijiografia eneo letu hili limekaa vibaya, ukanda wote wa Bahari ya Hindi ni eneo hatari. Eneo hatari kwa ugaidi, eneo hatari kwa maharamia, eneo hatari kwa kila vitisho vya kiusalama.”
Dk Bashiru alisema, “Vita ya rushwa si ya CCM au ya Rais Magufuli, ni vita ya Watanzania wote, rushwa ni adui wa haki, rushwa ni adui wa maendeleo na yote tunayoyafanya hatuwezi kuendelea kama tumefungwa minyororo na mafisadi.”
Alisema Taifa lilipofikia halipaswi kurudi nyuma au kukubali kuyumbishwa bali kuungana katika kuipigania nchi.
Katibu mkuu huyo alisema ni muhimu katika maonyesho hayo kuwapo na siku maalumu ya kutangaza amani na kudumisha umoja.
Dk Bashiru alitoa wito kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kutowaumiza wananchi wanaoishi jirani na hifadhi za Taifa na hasa wanapokuwa wakiwahamisha.
“Mnapokuwa mnataka kuwatoa wananchi msitumie nguvu, bali waelimisheni, msiwachomee nyumba na kuwapiga. Kwa kufanya hivyo mnachonganisha wananchi na chama, chama kipo kwa ajili ya kuwasaidia wananchi na si kuwachomea nyumba,” alisema Dk Bashiru.
Alisema, “Chama hakipendi kuona ng’ombe wa watu wanaswagwa, wananchi wanaharibiwa mali zao au wanapiga mayowe.”
Pia, alishauri Tantrade kuwa na siku maalumu ya kudumu ya kupambana na rushwa ambayo ni adui wa haki.
Post A Comment: