Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amezungumzia tena suala la baadhi ya watu kutoweka akiwemo mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda na msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Ben Saanane.

Lugola ameeleza kuwa jeshi la polisi linaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini uhalisia wa kutoonekana kwa watu hao na kwamba litatoa kauli yake baada ya kuthibitisha pasipo na shaka kuhusu kilichotokea.

Aliwataka Watanzania kuachana na uvumi usio na uthibitisho kuwa watu wanaotoweka wakiwa nyumbani kwao, kama ilivyokuwa kwa Azory wametekwa au kuuawa kwani Jeshi la Polisi ndilo lenye mamlaka kisheria kuthibisha hilo.

“Sio kila anayetoweka nyumbani kwake huwa ametekwa au kuuawa kama inavyovumishwa. Dhana hii inaniumiza na napenda watu waachane nayo,” anakaririwa na gazeti la Mwananchi.

“Tunaendelea kuchunguza kubaini sababu za kutoonekana kwao. Hauwezi kusema mtu amekufa bila kuwa na uthibitisho, na utathibitisha kwa kuuona mwili wake,” aliongeza.

Wazir Lugola aliongeza kuwa uchunguzi wa jeshi hilo ni kama jicho ambalo lina mwisho wa kuona, hivyo utakapofika mwisho wataeleza walichokibaini na mwisho kufanyia kazi jarada hilo ikiwa ni pamoja na kulifunga.

Ufafanuzi wa kauli ya Waziri Lugola umekuja ikiwa ni siku chache baada ya kuzua mijadala alipoeleza kuwa Serikali haiwezi kuingilia uhuru binafsi wa mtu kutoweka nyumbani kwake na kwenda anapotaka yeye.

Alisema watu wengi hufanya maamuzi yao wanapoona maisha yanawaendea visivyo, na huamua kwenda kuishi kokote watakapo na uamuzi wao huo unalindwa na Katiba ya nchi.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: