Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Phaustine Kasike ameahidi kutekeleza kikamilifu agizo la Rais John Magufuli aliyetaka wafungwa kuzalisha chakula kwa ajili ya kujilisha wakiwa gerezani.

Akizungumza leo Jumatatu Julai 16, 2018 wakati akikabidhiwa ofisi na Kamisha Jenerali mstaafu wa jeshi hilo, Juma Malewa amesema ataanzia pale alipoishia mtangulizi wake.

Katika hafla fupi ya kumuapisha Kasike iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, kiongozi mkuu huyo wa nchi alimtaka kutekeleza mambo mbalimbali, huku akimpongeza kidogo na kumpa pole.

Rais Magufuli alisema ni aibu Magereza kutegemea Bajeti ya Serikali wakati ina wafungwa wanaoweza kutumika kuzalisha chakula.

Kasike amesema tayari mtangulizi wake alishaanza kulifanyia kazi jambo hilo, yeye atakachokifanya ni kuendeleza alipoishia.

“Nitaendelea kuukamilisha mpango mkakati huu ili wafungwa kuanza uzalishaji na kujitegemea katika upande wa chakula,” amesema.

Amesema watawatengea kiasi cha fedha wafungwa watakaojishughulisha na uzalishaji ili wafanye shughuli hizo kwa ufanisi.

Kwa upande wake Malewa amesema,  “changamoto bado zipo nyingi, zingine zimeshafanyiwa kazi lakini kubwa  ni kwa hawa ambao tunawalinda ili wawe raia wema. Hivi sasa mbinu na matukio ya uhalifu yamebadilika, kwa uwezo wa Mungu utaweza kukabiliana nayo.”
Share To:

msumbanews

Post A Comment: