Wakazi wa mkoa wa Simiyu na mikoa ya jirani, wametakiwa kuchangamkia fursa zinazotokana na uwekezaji wa kampuni ya Kitalii ya Mwiba Holding Ltd ambayo imewekeza katika pori la akiba la Meatu linalopakana na Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro.
Akizungumza katika ziara ya kamati ya ulinzi na Usalama mkoa wa Simiyu na kamati ya Siasa ya CCM mkoa wa Simiyu na wilaya ya Meatu katika eneo la mwekezaji huyo, Mkuu wa mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka alisema uwekezaji wa kampuni hiyo umekuwa na faida kubwa kwa wananchi na taifa.
Mtaka alisema,kampuni hiyo ambayo imewekeza katika eneo la hifadhi ya Jamii ya wanyamapori(WMA) ya Makao na eneo la Ranchi kijiji cha Makao, licha ya kutoa malipo ya vijiji saba vinavyozunguka hifadhi hiyo kiasi cha sh 610 milioni kila mwaka pia anachangia misaada mingine ikiwepo kutoa ajira.
Alisema kampuni hiyo, pia imekuwa ikichangia shughuli za maendeleo na hivi karibuni, imetoa saruji mifugo 3000, mabati 1000 na zaidi ya sh 115 milioni kwa ajili ya kuchangia mfuko wa elimu wa mkoa.
“kama kulikuwa na mahusiano mabaya baina ya vijiji na serikali na wawekezaji hawa ambayo yalitokana na makosa ya watu wachache miaka ya nyuma sasa tumeanza ukurasa mpya”alisema
Awali Mmoja wa Wakurugenzi wa taasisi ya Friedkin Conservation Fund(FCF) ambayo kampuni zake ndizo zimewekeza katika wilaya hiyo ya Meatu, Abdulkadir Mohamed, alisema hadi sasa kampuni zao, Mwiba Holding, Tanzania Game Trackers Safaris(TGTS) na Wingert Safaris wamewekeza zaidi ya bilioni 670 na mwaka huu wataongeza sh 227 bilioni.
“tunatarajia kuongeza uwekezaji ila tunachoomba mazingira bora ya uwekezaji kuondolewa migogoro katika maeneo yetu, ikiwepo uvamizi wa mifugo na kama kuna mapungufu tuelezwe”alisema.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu,Enock Yakobo,alisema chama cha mapinduzi kwa sasa hakina mgogoro na wawekezaji kwani mapungufu yaliyokuwepo yamekwisha na mafanikio yanaonekana.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo, alishauri Mwekezaji huyo, kusaidia ujenzi wa mabweni kwa wanawafunzi wa kike katika shule ya Sekondari ya Makao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa chama cha wafugaji taifa, Jackson Yuma alitaka uongozi wa serikali kutokubali eneo la makao liharibiwe kwa kuruhusu mifugo kwani ndani ya mwaka mmoja hali itakuwa mbaya.
Yuma ambaye pia ni Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi wa CCM mkoa wa Simiyu, alitaka serikali kwa kushirikiana na wawekezaji kuhakikisha maeneo yaliyotengwa katika uhifadhi yanatunzwa kwa gharama zote kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo.
Post A Comment: