Kamati  Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inatarajiwa kukaa leo Dar es Salaam ambako pamoja na mambo mengine, inatarajiwa kujadili wabunge wa chama hicho ambao hawakuwapo bungeni wakati wa kupiga kura ya kupitisha bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 2018/19.

Kikao cha Kamati Kuu kitafanyika baada ya kile cha sekretarieti kilichofanyika jana chini ya uenyekiti wa Katibu Mkuu, Dk. Bashiru Ally, ambaye leo atawasilisha taarifa ya kikao hicho mbele ya wajumbe wa Kamati Kuu chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli.

Katika kikao cha sekretarieti masuala kadhaa yalijadiliwa, ikiwamo suala la utekelezaji wa ripoti ya Tume ya Uhakiki wa Mali za Chama iliyoongozwa na Dk. Bashiru.

Pia kilijadili utekelezaji wa ripoti hiyo na hatua za kuchukua baada ya Mwenyekiti wa CCM Rais Magufuli, kuagiza Katibu Mkuu kupitia sekretarieti afanyie kazi na kuchukua hatua haraka.

Pamoja na taarifa hiyo, pia kikao hicho cha Kamati Kuu kitajadili na kupitia jina la mgombea ubunge wa Buyungu katika uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Agosti 12 na mgombea wa nafasi ya uwakilishi Jimbo la Jang’ombe kisiwani Unguja baada ya aliyekuwa mwakilishi wake kuvuliwa uanachama wa CCM.

Taarifa za ndani zinaeleza kuwa baada ya kuwasilishwa taarifa ya Tume ya Uchunguzi wa Mali za Chama, Mei 21, mwaka huu, baadhi ya vigogo waliotajwa kwenye ripoti hiyo wameanza kurejesha magari na nyumba ambazo wanadaiwa kujimilikisha.

Pamoja na hali hiyo, inaelezwa kuna uwezekano mkubwa wa kufanyika kwa mabadiliko ya makatibu wa mikoa na wilaya wa CCM, hasa wale ambao ripoti ya uchunguzi imewagusa moja kwa moja.

Kwa wale ambao wameshindwa kurejesha mali hizo, sasa wamepewa barua za kutakiwa kuzirejesha na watakaposhindwa wapo hatarini kuburuzwa mahakamani.

Wakati hayo yakiendelea, kwa upande wa Zanzibar, jana Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, aliongoza kikao cha Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar mjini Unguja.

Kikao hicho kilikuwa na ajenda mbili, ambazo ni mapendekezo ya kupiga kura za maoni katika Uchaguzi wa Jimbo la Jang’ombe na mapendekezo ya wanachama wa CCM wanaoomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Uwakilishi katika jimbo hilo.

Wajumbe walimchagua Samia kuwa mwenyekiti wa muda na kuongoza kikao hicho kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM, Dk. Ali Mohammed Shein ambaye yupo safarini nje ya nchi.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: