Chama cha Wanasheria Tanganyika Law Society, kimelaani vikali kitendo kilichofanywa na mkuu wa mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti aliyetoa amri ya kukamatwa kwa mmoja ya wakili wao Menrad De Souza kitu ambacho ni kinyume cha Sheria ukizingatia hana mamlaka hiyo.

Akizungumza na Waandishi wa habari mapema leo jijini Dar- esa Salaam Rais wa chama hicho Fatma Karume amesema jana mchana mkuu huyo wa mkoa alimkamata mwanasheria wa chama hicho pamoja na wateja wake waliokwenda ofisini ili kuingia mkataba baina ya wateja na wakulima ndipo mkuu wa mkoa alipotoa amri kwa polisi mwanasheria huyo na wateja wake wakamatwe na kuwekwa ndani kwa masaa 48 kwa amri ya mkuu huyo wa mkoa.

Amesema chama hicho kimelazimika kutoa taarifa hiyo kwani siyo mara ya kwanza kwa wakuu wa mikoa na wilaya kutoa amri watu kuwekwa ndani na polisi kwa masaa 48, hivyo chama hicho kinapinga matumizi mabaya ya madaraka ya viongozi hao dhidi ya wananchi.

Fatma amesema hapa nchini hakuna mtu anayetoa hukumu ya mtu kukaa ndani isipokuwa Mahakama na hiyo ni baada ya kusikiliza pande zote mbili, hivyo wakuu wa wilaya na mikoa kutoa matamko ya kuwakamata watu ni sawa na kutoa hukumu jambo ambalo hawapaswi kufanya.

Ametumia fursa hiyo kueleza utofauti wa kisheria uliopo baina ya Zanzibar na Tanzania bara kwa kusema kuwa "Zanzibar huwezi kukaa ndani kwa miezi 9 bila kuhukumiwa hapo utapata dhamana moja kwa moja, hapa bara watu wanakaa miaka 9 mpaka 10 na hii ndio tofauti ya Sheria za Tanzania Bara na Zanzibar".

Ameongeza kuwa " Kuna changamoto kubwa sana kwa mawakili wetu kukaa ndani kwa muda mrefu, tatizo ni Tanzania Bara na sio Visiwani, bunge la huku Tanzania bara likipitisha Sheria siyo kwamba kesi hii hakuna kupata dhamana basi ndo imepita hapanaa hii ni sheria ovu".

Kwa upande wake wakili msomi Jebra Kambole amesema wakili huyo amekamatwa akiwa anatimiza majukumu yake ya kikazi, na kwamba Wakuu wa mikoa wamekuwa wakitumia sheria vibaya kuwaumiza wananchi na watu wengine kinyume na sheria.

"Kuna sheria na matumizi mabaya ya sheria, kwahiyo Wakuu wa mikoa wamekuwa wakitumia vibaya sheria na matokeo yake wanawaumiza wananchi, waandishi wa habari na wengine" ameongeza wakili Kambole.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: