Na Shabani Mdoe

KATIBU Mkuu wa CCM Dk.Bashiru Ally amekitumia salamu Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Arusha na kuwataka kujali zaidi maslahi ya Chama kwanza na si ya mtu binafsi ili kuwezesa malengo ya chama kufikiwa ikiwemo shabaha ya kushika dola.

Amewataka viongozi na wanachama mkoani hapa kuweka tofauti zao kando hasa katika kipindi hichi cha uchaguzi mdogo wa marudio wa udiwani ambapo kwa mkoa wa Arusha pekee una jumla ya kata 20 zinazofanya uchaguzi kufuatia madiwani 19 waliokua wa Chama Cha Chadema kujiuzulu nafasi zao na mmoja kufariki dunia.

Akiwasilisha salamu hizo za Dk.Bashiru kwenye kikao maalumu cha halmashaauri kuu ya mkoa kilichoketi kwa lengo la kuteua majina ya wagombea wa udiwani  katika kata hizo 20 katibu wa CCM mkoa wa Arusha Elias Mpanda alisema alipokea salamu hizo siku hiyo asubuhi kabla ya kikao kuanza.

Mpanda alisema Dk.Bashiru alielekeza kuwa katika kipindi hichi cha uchaguzi hata kama kiongozi au mwanachama hampeni mwenzie si wakati wake bali kwasasa wanapaswa kutofautisha chuki zao binafsi na chama kwa lengo moja la kufanikisha ushindi wa chama chao.

Alisema kwa salamu hizo wana CCM wa Mkoa wa Arusha wanapaswa kuziheshimu na kutekeleza kwasasa wakati wa uchaguzi na hata baada ya uchaguzi kwani ushindi wa chama hautafutwi katika kipindi cha kampeni tu bali hata mara baada ya uchaguzi na kabla ya uhaguzi kwa kuwepo kwa ushirikiano.

Naye mwenyekiti wa CCM mkoa wa Arusha Loata Sanare alisifu kuanza kuonekana kwa ushirikiano baina ya wanachama kwa wanachama na hata viongozi kwa viongozi jambo ambalo anaamini litaweza kuleta ushindi kwa chama hasa katika chaguzi za kata 20.

Aliwataka wajumbe wa hao wa halmashauri kuu ya mkoa kutambua kuwa Arusha ndiyo yenye kata nyingi za uchaguzi kuliko mkoa mwingine wowote lakini pia mbali na wingi wa kata hizo pia uchaguzi wa mkoa wa Arusha unaangaliwa kwa macho manne kutokana na aina ya siasa iliyoko katika mkoa huo.

Alisema hata viongozi wa chama ngazi ya kitaifa pamoja na kuwepo kwa chaguzi kwa mikoa yote nchini lakini tazamio lao kubwa ni kwa mkoa wa Arusha hasa ukizingatia mgombea wa Urais kwa tiketi ya Ukawa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 Edward Lowasa anatokea mkoa huu wa Arusha.

Kikao hicho cha halmashauri kuu ya mkoa pamoja na mambo mengine kiliazimia kwa pamoja kujipanga vyema katika kuhakikisha chama kinapata ushindi wa kishindo kwa kata zote 20 ili kujihakikishia kazi rahisi wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa hapo mwakani.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: