Tarime - Mara: WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ameliagiza Jeshi la Polisi wilaya ya Tarime mkoani Mara kumkamata na kumfungulia mashtaka Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) wa Wilaya hiyo, Newton Mongi na Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya wilaya hiyo, Richard Tiboche kwa tuhuma za kuikashifu Serikali na kuchochea mgogoro wa mpaka kati ya hifadhi ya Serengeti na vijiji jirani.

Dk. Kigwangalla ametoa agizo hilo jana majira ya saa tatu usiku baada ya kuhitimisha ziara yake wilayani humo iliyolenga kutafuta suluhu ya mgogoro uliodumu kwa miongo kadhaa kuhusu mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na vijiji jirani ikiwemo kijiji cha Kegonga.

Akiwa njiani majira ya saa tatu za usiku kwenye gari la wazi baada ya kukagua eneo hilo la mpaka kwa zaidi ya masaa sita, Waziri Kigwangalla na msafara wake walikuta lundo la mawe yakiwa barabarani ndani ya eneo la hifadhi hiyo, hali iliyosababisha taharuki kubwa na msafara wake kushuka na kuanza kuondoa mawe hayo ili kupata njia ya kupita.

Wakati zoezi hilo likiwa  linaendelea, Kiongozi huyo wa UVCCM alisikika akiituhumu Serikali kwa kuweka mawe hayo na kwamba hayakuwekwa na wananchi wa eneo hilo, jambo lililozua mshangao mkubwa  kwa viongozi wa Serikali waliokuwepo katika msafara huo akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima.

Mkuu huyo wa mkoa alisema tukio hilo sio la mara ya kwanza na kwamba limewahi kuripotiwa mara nyingi na uongozi wa hifadhi hiyo kuwa wananchi wa vijiji jirani hujaza mawe barabarani kwa ajili ya kuzuia magari ya doria ili waweze kulisha mifugo yao ndani ya hifadhi hiyo. Alisema hata msafara wa tume ya Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda iliyoundwa na CCM hivi karibuni kufuatilia mgogoro katika eneo hilo nao ulizuiliwa kwa mawe barabarani.

Imedaiwa pia kuwa kwa nyakati tofauti viongozi hao wamekuwa wakiwatolea viongozi wa Serikali maneno ya kejeli pamoja na kuwakwamisha kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi ipasavyo.

Awali, kabla ya tukio hilo la mawe barabarani moja ya gari lililokuwa likiongoza msafara huo lilipata pancha baada ya kukanyaga misumari iliyokuwa imetengwa kwenye moja ya barabara zinazoingia na kutoka ndani ya Hifadhi ya hiyo ya Serengeti.

Waziri Kigwangalla alisikitishwa na kitendo hicho ambacho alikielezea kuwa sio cha kiuungwana kwa kuwa kinalenga kudhoofisha juhudi za Serikali kumaliza mgogoro huo kwa faida ya pande zote.

"Mimi ni Muislam, nimesikia kwa masikio yangu na wala sijaambiwa na mtu yeyote na siwezi kumsingizia mtu, nimeshangazwa sana na kiongozi tena mtendaji wa chama tawala anawezaje kuitukana Serikali, na hapa sisi tumekuja kuwahudumia wananchi" alisema Dk. Kigwangalla kwa masikitiko makubwa.

Wakati huo huo, Waziri Kigwangalla ametoa miezi mitatu kwa wananchi wote waliovamia ndani ya Hifadhi ya Serengeti na eneo la wazi (buffer zone) ambao wanaendesha shughuli zao ikiwemo kilimo, ufugaji na makazi kuachia maeneo hayo kwa hiari yao wenyewe, na kwamba muda huo ukipita wataondolewa kwa nguvu na chochote kitakachokutwa ndani ya eneo hilo kitatekezwa kwa mujibu wa sheria.

Akizungumzia kuhusu suluhu ya mgogoro huo wa mpaka amesema, Serikali itaunda timu ya wataalam kutoka wizarani kwake, wizara ya ardhi, uongozi wa mkoa wa Mara na wilaya ya Tarime ambao watashirikiana na watu wengine huru watakaochaguliwa na wananchi wa vjiji husika wakiongozwa na mbunge wao, John Heche ambao watakuwa na uelewa wa kusoma ramani na kutafsiri mipaka ili kushirikiana kuhakiki mipaka halisi ya eneo hilo na kufikia muafaka.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: