Kitendo cha gari la wagonjwa kukamatwa likiwa limebeba dawa za kulevya aina ya mirungi, limeendelea kuwa gumzo kila kona huku Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mara, kikilaani jambo hilo.
Gari hilo linalotumiwa na hospitali ya wilaya ya Tarime, lilikamatwa Jumatano wiki hii wilayani Bunda likiwa na shehena ya kilo 823 za mirungi iliyokuwa ndani ya magunia.
Kutokana hatua hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, juzi alitangaza kuwasimamisha kazi watumishi watatu wa hospitali hiyo akiwamo Mganga Mkuu wa Halmashauri, Dk. Innocent Kweka.
Wengine waliokumbwa na hatua hiyo ni Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali, Dk. Hamili Kombo na Katibu wa Afya, Rwegasira Karugwa. Sababu kubwa ya kusimamishwa kwao ni uzembe.
Kitendo hicho kimeiamsha CCM mkoa na kutaka serikali kufanya uchunguzi wa kina ili kuwabaini watu wote walioko kwenye mtandao huo, na hatimaye kuchukuliwa hatua stahiki za kinidhamu ikiwamo kufikishwa mahakamani.
Mwenyekiti wa CCM mkoani hapa, Samuel Kiboye, alisema kikao cha Halmashauri Kuu ya Mkoa kilichofanyika jana mjini hapa, kimetoa tamko hilo ili kuonyesha kuwa hakikubaliani na kitendo hicho .
Kiboye alisema kitendo cha gari la wagonjwa kubeba dawa za kulevya hakiwezi kuvumiliwa na kinapaswa kulaaniwa na kila mwananchi kwa sababu kimeleta aibu kwa wilaya ya Tarime, mkoa wa Mara na Tanzania kwa ujumla.
“Sisi wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM mkoani wa Mara, kwa ujumla tunalaani kitendo cha gari la wagonjwa kubeba dawa za kulevya maana kimetupa aibu sana wananchi wote wa mkoa wa Mara. Tunakuomba Mkuu wa Mkoa (Adam Malima) muwakamate wote waliohuska. Fanyeni uchunguzi wa kina kwani huenda wamo pia viongozi wa serikali,” alisema.
Naye Malima alisema serikali itahakikisha wote walioko kwenye mtandao huo wanakamatwa na kwamba tayari watuhumiwa wawili, akiwemo dereva wa gari hilo, George Matai, wanashikiliwa na polisi na kuongeza kuwa uchunguzi zaidi juu ya suala hilo bado unaendelea.
Gari hilo la wagonjwa lenye namba za usajili DFPA 2955, lilikamatwa na polisi wa wilayani Tarime, katika kijiji cha Bitaraguru wilayani Bunda, likiwa limepakia magunia 34 ya dawa za kulevya zenye uzito wa zaidi ya tani 800.
Askari hao walikuwa wanatoka wilayani Tarime wakiwa wanapeleka mgonjwa ambaye ni askari mwenzao katika Hospitali ya Rufani ya Bugando jijini Mwanza, aliyejeruhiwa kichwani baada ya kupata ajali ya pikipiki.
Post A Comment: