Matokeo mabaya ya kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Jangwani, jijini Dar es Salaam, yamesababisha walimu 48, akiwamo Mkuu wa Shule hiyo, Geraldine Mwaisenga, kuondolewa.

Mbali na walimu hao, serikali pia imetangaza kuwaondoa walinzi wote waliokuwapo pamoja na watumishi ambao hawakuwa walimu ikiwa ni jitihada za kuinusuru shule hiyo inayozidi kuporomoka kielimu.

Katika matokeo ya kidato cha sita yaliyotangazwa hivi karibuni na Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania (Necta) na kuwa gumzo miongoni mwa wadau wa elimu, shule hiyo kongwe ilishika moja kati ya nafasi 10 za mwisho. Kwa mujibu wa matokeo hayo, Shule hiyo ilikuwa ya 451 kati ya 453 zilizofanya mtihani huo.

Hatua ya shule hiyo kuwa mkiani kwenye matokeo hayo, ilisababisha Waziri wa elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Ndalichako, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, kufika shuleni hapo na kutoa ya moyoni.

Jafo katika ziara yake shuleni hapo, bila kuuma maneno, alisema sababu zilizofanya kupatikana kwa matokeo hayo mabaya ni udhaifu katika uongozi wa shule, uasherati miongoni mwa wanafunzi na walimu kufika na kutia saini kisha kuondoka na kwenda kufanya shughuli zao binafsi.

Akitangaza uamuzi huo jana wakati akizungumza na kituo kimoja cha televisheni , Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresia Mmbando, alisema hatua hizo zimechukuliwa kuinusuru shule hiyo kongwe nchini.

Alisema shule hiyo ilikuwa na walimu 87, hivyo baada ya kuwaondoa 48 ambao ni zaidi ya nusu ya waliokuwapo serikali itahakikisha inaiongezea shule hiyo walimu angalau wengine 20.

“Tumewaondoa pia watumishi wasio walimu wakiwamo walinzi ambao walibainika kuwa ni kikwazo na walichangia kwa namna mbalimbali wanafunzi kufeli,” alisema.

“Tunahakikisha tunabadilisha utawala mzima na baadhi ya watumishi ili kuimarisha uongozi na usimamizi. Lengo ni kuhakikisha shule hiyo inafanya vizuri kwenye matokeo ya kidato cha nne na cha sita,” alisema.

Pia alisema serikali imeweka mkakati kuhakikisha wanafunzi wa shule hiyo wanakuwa na nidhamu inayotakiwa ili kufanya vyema kwenye mitihani.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: