Mbunge wa Kigoma Mjini, Bw. Zitto Zuberi Kabwe leo bungeni ametoa taarifa kwa Wabunge wenzake pamoja na Mwenyekiti wa Bunge hilo Mussa Azzan Zungu kwamba atatoa hoja binafsi kutaka bunge kuunda kamati teule ya kufanya uchunguzi kuhusu mauaji mbalimbali zilizojitokeza katola Mkoa wa Pwani.
Zitto ameyasema hayo kwenye sehemu ya tatu ya hotuba yake juu ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa Mwaka 2018/19.
Katika hotuba yake Zitto amesema kwamba zaidi ya Watanzania 380 wanatajwa ‘kupotezwa’ MKIRU, (Mkuranga, Kibiti na Rufiji) Bunge lichunguze kama lilivyochunguza Operesheni Tokomeza.
"Naomba kutoa Taarifa kwamba nitatoa hoja binafsi kutaka Bunge lako Tukufu kuunda Kamati Teule kufanya uchunguzi kuhusu kadhia za Mauaji, Kupotea, Kupigwa Risasi, Kuteswa watu wa MKIRU na Kusini kwa ujumla. Ni imani yangu kuwa Wabunge wenzangu mtaunga mkono jambo hili. Zitto Kabwe.
Ameongeza kuwa "Kadhia za namna hii ni nyingi mno, na yeyote kati yetu, akipata wasaa tu wa kwenda MKIRU (Mkuranga, Kibiti na Rufiji) ataelezwa mambo haya kwa undani, makadirio ni kuwa zipo kesi zaidi ya 380 za namna hii za watu kuchukuliwa na kutorudishwa kwa zaidi ya miezi 10 sasa, hizo ni tofauti na zile za watu waliokamatwa, kuteswa na kisha kuachiwa, au wale waliojeruhiwa kwa kupigwa risasi".
"Na si MKIRU tu, bali ukanda wote wa Kusini, wiki mbili zilizopita, Mbunge wa Kilwa Kusini, Mh. Suleiman Bungara ‘Bwege’ (CUF) naye alieleza kadhia za watu 10 wa Jimboni kwake Kilwa, kuchukuliwa Msikitini na Jeshi letu la Polisi, kupigwa risasi, wengine kutokurudishwa mpaka leo, na kuhisiwa kuwa wameuawa, wengine kurudishwa wakiwa na vilema vya kukatwa masikio, kuchomwa ndevu kwa moto".
Post A Comment: