Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Zuberi Kabwe amesema kwamba haiingii akilini kwa serikali kuagiza malighafi za kujengea reli nchini, wakati tuna makaa ya mawe na chuma wilayani Ludewa, ambayo mpaka sasa hayajaanza kuchimbwa.

Akizungumza Bungeni jana Zitto Kabwe alisema iwapo serikali ingechukua hatua katika kutengeneza kiwanda cha chuma kutokana na madini ya chuma yaliyopo Ludewa, serikali isingeingia gharama ya kuagiza malighafi za ujenzi wa reli nje, na pia ingeweza kupata kipato kwa kuuza kwa nchi jirani kama Kenya na Zambia, ambako nako kuna ujenzi wa reli unaendelea.

“Niligusia ujenzi wa reli na jinsi ambayo tunaagiza malighafi za ujenzi kutoka nje, waziri anasema wameenda wamezindua kiwanda cha nondo sijui wapi na wapi, nondo zote hizi malighafi zake ni kutoka nje, na tuna chuma Mchuchuma na Liganga miaka yote hii. 

"Kweli inaingia akilini tuna chuma na makaa ya mawe yamejaa pale Ludewa, tunampa mkandarasi kazi ya kujenga reli, vyuma vinatoka Uturuki, India, China kweli Mh. Spika!!? Kenya nao wanajenga reli tungeweza kuwauzia”, alisema Zitto Kabwe.

Sambamba na hilo Zitto Kabwe amesema nchi inatia aibu kuagiza mafuta kutoka nje na kuibua mgogoro mkubwa kuhusu bidhaa hiyo, wakati nchi ina rasilimali za kutosha za kutengeneza mafuta, ila haijaweka mikakati wala mipango yoyote kukuza sekta hiyo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: