Serikali ya Zanzibar imeagiza zaidi ya waalimu 300 wa masomo ya Sayansi kutoka nchini Nigeria ambao tayari wameanza kuwasili visiwani humo.
Kwa mujibu wa serikali ya Zanzibar, waalimu hao wanaoingia kwa awamu, na wanatarajiwa kuziba pengo la uhitaji wa zaidi ya waalimu 300 wa masomo hayo.
Naibu waziri wa Elimu Zanzibar Mmanga Mjengo amesema ujio huo utasaidia kuamsha pia morali ya waalimu wengine wa masomo ya sayansi visiwani humo.
Ameongeza pia wameamua kwenda Nchini Nigeria kwa sababu kuna wingi wa waalimu na wenye ubora na haikuwa rahisi kuchukua kutoka nchi za karibu kwa sababu na wao pia wana tatizo la uhaba wa waalimu.
''Mchakato wa upatikanaji wa waalimu hawa hufanywa kwa kutegemea uwezo wao katika ufundishaji na pia ubora wa kazi zao.'' alisema waziri Mjengo.
Serikali ya Zanzibar imesisitiza kuwa sio mara ya kwanza kwa ujio kama huu kwani katika miaka ya nyuma waalimu hawa wamekua wakija kwa kujitolea.
Ujio wa waalimu hawa ambao watakuwepo kwa kipindi cha miaka miwili unatajwa kupunguza uhitaji wa zaidi ya waalimu 300 visiwani humo.
Post A Comment: