Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia kwa Waziri wake Mhe. Dkt. Hamisi A. Kigwangalla, imekanusha habari za uzushi zilizoripotiwa na Taasisi ya Oakland iliyopo Marekani juu ya nchi ya Tanzania kukandamiza haki za Wamaasai wanaoishi Loliondo, mkoani Arusha.
Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa siku ya jana Mei 10, 2018, waziri Kigwangalla amesema kuwa taarifa ya Oakland iliyopewa kichwa cha habari “Losing the Serengeti: The Maasai land that was to run forever”, ambayo imeituhumu serikali ya Tanzania kuwa imechoma makazi ya jamii ya wamasai na kuondoa mifugo yao kwenye maeneo ya malisho ya maji, ni potofu na haina ukweli wowote.
Kwa mujibu wa Kigwangalla, taarifa hiyo pia ambayo ilinukuliwa na Shirika la Utangazaji BBC kwa kichwa cha habari “Tanzania yadaiwa kukandamiza haki za Wamaasai wanaoishi Loliondo”, inalenga kuipaka matope serikali na kuleta uchonganishi baina yake na wananchi pamoja na wawekezaji, huku akisema kuwa serikali inaendelea kutatua mgogoro uliopo katika eneo la Loliondo na kuwa itatoa taarifa rasmi hapo baadae.
Amesema kutokana na umuhimu wa eneo hilo kwa uhifadhi, uwepo wa vyanzo vya maji, eneo la mzunguko wa uhamiaji wa wanyamapori na maisha ya watu, serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu ilichukua hatua stahiki za kutatua mgogoro huo.
Kigwangalla amehitimisha taarifa yake kwa kusema kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kushirikiana na wadau wenye nia njema kwa uhifadhi na maendeleo ya wananchi katika kusimamia na kuendeleza rasilimali zilizopo katika eneo la Loliondo na maeneo mengine nchini kwa maslahi mapana ya Taifa.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: