Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako ameagiza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Baraza la Vyuo vya Ufundi (Nacte) kufanya mapitio upya ya nyenzo wanazotumia kukagulia ubora wa vyuo.
Profesa Ndalichako amesema vikibainika havina ubora wavifungie mara moja hata kama ni vya Serikali.
Akijibu hoja za wabunge leo Mei 2, 2018 bungeni mjini Dodoma walipojadili bajeti ya wizara yake ya mwaka 2018/19 amesema kuna baadhi ya wabunge wamelalamikia kuhusu wahitimu wa vyuo kushindwa kuandika wasifu.
“Nacte na TCU wamekuwa wakifungia vyuo vingi sana, lakini tatizo badi lipo, kwa hiyo naviagiza vyombo vya udhibiti wa elimu kufanyia mapitio upya ya nyenzo za ukaguzi ikiwemo sifa za walimu, mitihani inayotolewa na usahihishaji wao,” amesema Profesa Ndalichako.
“Iwapo watabaini havikukidhi ubora wavifungie bila kuogopa mtu yeyote hata kama vikiwa vya Serikali, vifungiwe.” ameongeza
Waziri huyo amewaagiza maofisa elimu nchini kusimamia kwa karibu ubora wa elimu katika shule zilizopo katika maeneo yao huku akidai kitendo cha kumfukuza mwalimu mkuu na kumuacha ofisa elimu wa eneo husika ni uonevu kwa sababu wao ndiyo wanapaswa kusimamia ubora wa elimu.
“Utakuta ofisa elimu ana shule tano tu lakini anashindwa kuzisimamia na Serikali haitakubali kuwa na viongozi mizigo,” amesisitiza Waziri huyo.
Post A Comment: