Na: Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim  Majaliwa ameiagiza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kukaa pamoja na chama cha wapangaji wa nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ili kusikiliza changamoto zao pamoja na kutoa fursa kwa wapangaji wa muda mrefu kununua nyumba hizo.

Mhe. Majaliwa ametoa tamko hilo leo Bungeni, Jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Ilala Mhe. Azzan Mussa Zungu juu ya lini Serikali itakutana na wanachama na wamiliki wa nyumba za NHC ili kutoa fursa kwa wapangaji wa muda mrefu kuzinunua nyumba hizo badala ya kuwaondoa.

“Shirika la nyumba inayo sera inayotoa muongozo namna nyumba hizo zinavyotakiwa kutumika ikiwemo na maamuzi kwa wale wanaokaa kwa muda mrefu kwenye nyumba hizo inapofikia thamani ya nyumba kushuka iweze kurasimishwa rasmi ili kutoa fursa kwa wapangaji hao kuweza kuzinunua kwa kulipa kiwango kidogo kidogo,” alisema Waziri Mkuu.

Aliendele kusema, asilimia kubwa ya wapangaji wa muda mrefu wa nyumba hizo ni wastaafu ambao hawana nyumba. Hivyo ameitaka NHC kuangalia jambo hilo na kuwapa fursa wapangaji hao kulipa kidogo kidogo kadiri ya uwezo wao.

Wakati huo huo Waziri Mkuu ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutotumia lugha ya kuudhi au kutumia nguvu pindi wanapokusanya kodi kwa wafanyabiashara. Badala yake wawaelimisha wafanyabiashara juu ya umuhimu wa kulipa kodi na kuwaeleza ni kwa kiasi gani kodi hiyo imefikia.

Amesema hayo, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Tunduma Mhe. Frank Mwakajoka kuhusu kauli ya Serikali juu ya usumbufu unaoletwa na TRA kwa wafanyabiashara wakati wa kukusanya kodi.

“Serikali imeunda chombo cha kusikiliza kero za wananchi ndani ya TRA lakini kama hawatasikilizwa wanauwezo wa kupeleka kero zao Wizara ya Fedha au kwa kiongozi yoyote mkubwa katika eneo lake kama vile Mkuu wa Mkoa au Wilaya,” alisema Waziri Mkuu.

Aidha ameitaka Mamlaka hiyo kufanya kazi kwa weledi na kuwa na mazungumzo na wafanyabiara. Pia tathmini ya kodi isiwe kiwango kikubwa kuliko mtaji wa mfanyabiashara.

Hata hivyo amesema hatua zitachukuliwa kwa yeyote ambaye hatatumia utaratibu mzuri wa kukusanya  kodi na amewataka wafanyabiashara kufanya biashara kwa amani
Share To:

msumbanews

Post A Comment: