Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi amesema masheikh wa Uamsho kuchelewa kufikishwa mahakamani kunatokana na upelelezi kutokamilika, kwamba Serikali imeomba ushahidi kutoka nje ya nchi.

Akizungumza jana  wakati akijibu hoja  za wabunge zilizoibuka wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi mwaka 2018/19, Kabudi amesema suala hilo halihusu wizara hiyo, kwamba linamhusu Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

“DPP ana uwezo wa kufungua mashtaka na kuyafuta na hakuna mtu wa kuingilia . Na kwa sababu hawezi kuingia bungeni nimemwomba anipe majibu kuhusu suala la masheikh wa uamsho.  DPP alikuwa Singida nimemuomba aje aniletee taarifa hapa,”amlisema.

Alisema kuwa suala hilo ni nyeti na adhabu yake ni kubwa, hivyo ndio maana upelelezi umechukua muda mrefu ili kuhakikisha wanapata taarifa za kutosha kabla ya kuwafikisha mahakamani.

Hata hivyo, alisema Serikali ina nia ya dhati ya kuhakikisha suala hilo linafikia mwisho.

“Na hii bahati mbaya sana watu wanaojadiliwa wana hadhi ya masheikh lakini hawakuingizwa kwenye tuhuma za ugaidi kama masheikh, kwa sababu tuhuma lazima tuchunguze kwani wakitiwa hatiani adhabu yake ni kubwa,”alisema.

Alisema uchunguzi huo unafanyika nje ya nchi na ndani ya nchi na kwamba wameomba ushahidi kutoka nje ya nchi kuhusiana na tuhuma hizo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: