Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amewataka askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani kujitafakari kuhusu faini wanazotoza na kuacha kubambikiza kesi kwa madereva.
Akijibu hoja za wabunge walizozitoa wakati wakichangia bajeti ya wizara hiyo mwaka 2018/19 jana Mei 4, 2018 bungeni mjini Dodoma, Masauni amesema chanzo kikubwa cha ajali barabarani ni pamoja na makosa ya kibinadamu kwa asilimia 76, ubovu wa miundombinu na uchakavu wa magari.
“Bado kuna changamoto za baadhi ya madereva ambao hawafuati sheria. Trafiki acheni tabia za aina hiyo, watu hawajafunga mkanda badala ya kumwelewesha unamtoza faini,”alisema.
“Lazima waangalie uzito wa kosa lenyewe na wafanye kwa mujibu wa sheria. Kama mtu hajafunga mkanda unamtoza faini badala ya kumpa elimu tu. Raia nao wawape ushirikiano askari wetu kwani wanafanaya kazi katika mazingira magumu zaidi.”
Amlisema serikali kwa upande wake inafanya kila juhudi ikiwemo kupata mkopo mkubwa kutoka Benki ya Exim wa Sh500 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Serikali ambapo kila nyumba itajengwa kwa gharama ya Sh25 milioni.
Kuhusu uhamiaji, Masauni amesema Serikali imefanikiwa kufumua mtandao wa watendaji wa idara ya uhamiaji mikoani ambao hawakuwa waaminifu katika utendaji wao wa kazi.
Ameahidi kufanya kila namna ya kuwasaidia wananchi wa mkoa wa Kigoma ambao wamekuwa wakilalamika kuhusu utendaji wa idara hiyo kwa kila wakati kuulizwa kuhusu vitambulisho.
Post A Comment: