Siku moja baada ya Rais John Magufuli kuahidi kupandisha mishahara ya watumishi baada ya uchumi kutengamaa, wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Sixtus Mapunda(Mbinga Mjini) na Musa Sima (Singida Mjini), wameitaka serikali kueleza ni lini mishahara hiyo itapanda.
Wabunge hao wamehoji hayo leo Mei 2, bungeni jijini Dodoma baada ya kuomba muongozo kwa mwenyekiti wa Bunge Andrew Chenge kuhusu majibu ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji kuhusu mipango ya serikali kupunguza umaskini.
Mapunda amesema katika swali namba 166 lililoulizwa na Mbunge wa Kasulu Mjini, Daniel Nsanzugwanko, majibu ya serikali katika ujumla wake yalijikita kwenye kuondoa umaskini wa kipato na kwa kuwa umaskini wa kipato una uhusiano moja kwa moja na ongezeko la mishahara ya watumishi wa serikali wa kada zote.
“Kwa kuwa jana rais alisema kuwa ongezeko la mishahara pamoja na mambo mengine litazingatia hali halisi ya uchumi uwezo wa serikali kulipa na mahitaji halisi ya serikali, na kwa kuwa rais ameshaji-commit kuwa kutakuwa na ongezeko la mishahara litakalozingatia mahitaji ya msingi, serikali inatoa kauli gani, lini ni mishahara hiyo itapanda maana hili suala ni kama lipo hewani na limeacha sitofahamu nyingi kwa wananchi,” alihoji Mapunda.
Kwa upande wake Musa Sima naye aliomba mwongozo na kueleza kuwa Dk. Kijaji anatoa majibu kuhusu miongoni mwa hatua za kuondoa umaskini Tanzania hakuweza kuonesha nyongeza ya mishahara kwa watumishi.
“Sasa nimpongeze rais kwa hotuba yake ya Mei mosi, lakini ni vizuri kama Bunge tukahitaji kusikia kauli ya serikali kwa ajili ya watumishi ni lini sasa serikali itahakikisha itapandisha mishahara ya watumishi hawa kama hatua mojawapo ya kuondoa umasikini?,” aliuliza Sima.
Akijibu miongozo hiyo, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge aliitaka serikali kujipatia nafasi nzuri nzuri ya kujielezea na kuwapa matumaini wananchi.
“Kwa kuwa ni swali ambalo linahusu na maslahi ya wafanyakazi wa Watanzania, ndiyo maana limelengwa na Mapunda na Sima, nadhani serikali mnaweza kupata nafasi nzuri ya kujielezea na kuwapa matumaini wananchi.
“Ni lini, hayo ni maswali sasa tunaiachia serikali hadi hali ya uchumi itakaporuhusu, tufanye haya makubwa yatakayowezesha kukuza uchumi wetu kwa haraka siri ya maendeleo ni hiyo tu, tufanye kazi kwa bidii tukuze uchumi, lakini serikali nadhani kwa wakati muafaka wanaweza kulitolea maelezo,” amesema Chenge.
Post A Comment: