Mbunge wa Kuteuliwa, Abdallah Bulembo, amehoji bungeni mjini Dodoma kwa nini baadhi ya askari polisi wana vitambi vikubwa.
Bulembo alitoa hoja hiyo jana alipokuwa ananchangia mjadala wa makadirio ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka ujao wa fedha.
Alihoji sababu za baadhi ya askari kuwa na vitambi vikubwa, akidai vinasababisha washindwe kufanya mazoezi ya kiaskari.
Mbunge huyo pia aliishukia Idara ya Uhamiaji akidai imekuwa ikihangaika na wahamiaji haramu wanaopita kutoka nje huku ikiwalinda walioko ndani ya nchi.
Alisema pamoja na idara hiyo kufanya kazi nzuri, imekuwa ikishughulikia sana wahamiaji na hasa wale wa kutoka Ethiopia.
Bulembo ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) hadi mwishoni mwa mwaka jana, alisema wakati wakifanya hivyo, wamekuwa wakiwalinda wahamiaji ambao wamo ndani ya nchi na wengine wameishi zaidi ya miaka 20 sasa bila kuwa na vibali maalum.
Alisema hali hiyo ni hatari kwa kuwa wengine wamekuwa wakilindwa na watendaji toka idara hiyo na wanaendesha shughuli zao bila wasiwasi.
“Inashangaza kuna baadhi ya wahindi wapo humu nchini zaidi ya miaka 20 na wanajulikana lakini mnawaacha na badala yake mnawakamata kina Bashe ambao wamezaliwa hapa nchini,” alisema.
Bulembo pia alizungumza kuhusu utendaji wa Kikosi cha Usalama Barabarani akieleza kuwa kumekuwa na tabia ya baadhi ya wabunge kutumia ubunge wao kama kinga dhidi ya kikosi hicho wanapofanya makosa ya barabarani.
Alisema ni vyema kikosi hicho kikafanya kazi yake kama ilivyopangwa na si kuogopa pale kinapowakamata wabunge.
“Kama mbunge kafanya kosa, kamata peleka mahakamani. Ubunge siyo kinga ya kufanya makosa na wala isiwe kuwatishia askari wa barabarani, waacheni wafanye kazi zao,’’ alisema.
Naye Mbunge wa Mkokotoni, Juma Othman Hija (CCM), alisema kumekuwa na uhaba mkubwa wa nyumba za askari katika jimbo lake ambalo pia linakabiliwa na changamoto ya uchakavu wa vituo vya polisi.
Alisema kutokana na uchakavu huo, askari polisi wakati wa mvua wamekuwa wanalazimika kufanya kazi zao katika chumba cha mahabusu.Alisema hali hiyo ni aibu kwa Jeshi la Polisi kwa kuwa wananchi wengi wanawategemea kufanya kazi ya kuwalinda, lakini linakosa ofisi bora na vitendea kazi.
Alisema jeshi hilo pia linakabiliwa na uhaba wa karatasi akidai kuwa yeye binafsi alikwenda kwenye Kituo cha Polisi cha Kati mjini hapa na alichukuliwa maelezo kwa kutumia karatasi zinazotumika kwa ajili ya shughuli za Bunge.
Post A Comment: