KIMENUKA! Muuza sura kwenye video mbalimbali za wasanii wa Bongo Fleva, Tunda Sebastian ‘Tunda’ amelikoleza bifu lake na mwanamitindo Hamisa Mobeto baada ya kumpa mashuti kuwa amejidhalilisha kurudiana na msanii wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.
Kwa mujibu wa chanzo makini, Tunda ambaye aliwahi kuripotiwa kutoka kimapenzi na Diamond, amechukizwa na kitendo cha Mobeto kujipeleka kwa msanii huyo wakati kipindi cha nyuma alishawahi kumdhalilisha.
“Ujue tangu siku ile ya uzinduzi wa Tuzo za Sinema Zetu pale Mlimani City Mobeto alipoweka wazi mwanaume anayemkubali ni Diamond tena wakaenda mbele ya jukwaa kukabidhi tuzo wakikumbatiana kimahaba, Tunda amekuwa akimchukia sana Mobeto na kumuona kama mwanamke asiyejielewa,” kilisema chanzo.
Chanzo kiliendelea kumwaga ubuyu kuwa, kinachomuumiza zaidi Tunda ni hapo nyuma Mobeto alishawahi kumdhalilisha msanii huyo anayetamba na Wimbo wa African Beauty kwa kumtafutia mwanasheria kudai malezi ya mtoto waliozaa naye mahakamani.
“Anajua kabisa alishampeleka Diamond hadi mahakamani kudai malezi ya mtoto na wakaafikiana lakini bado ameendelea kumng’ang’ana tu,” chanzo kiliweka nukta.
Ijumaa lilimtafuta Tunda na kuulizwa juu ya bifu hilo ambapo alilikoleza kwa kumpa Mobeto mashuti ya kufa mtu.
“Huyo Mobeto kazidi, yaani kwanza amekubali kudhalilishwa kwenye ile video ya nusu utupu kisa tu aonekane yupo na Diamond ingekuwa ni mimi wala nisingekubali kudhalilishwa huko.
“Nashangaa sijui kwa nini wanawake wengine wanapenda sana kudhalilishwa, hebu fikiria juzi tu ameenda hadi kumshtaki mwenzake juu ya bwana huyo jua ya malezi ya mtoto lakini leo kasahau yote na kachezewa na video chafu, ametukanwa weee lakini bado yupo tu tena anajiona mjanja,” alisema Tunda.
Tunda alipoulizwa mashuti hayo labda ni kwa sababu aliwahi kutoka na Diamond hivyo anaona wivu alisema;
“Wala sisemi kwa maana hiyo ila huyo mwanamke kazidi bwana! Nashangaa sana kwa mwanamke kuwa hivyo hasa akiwa staa.”
Ili kuweka mzani sawa, Ijumaa lilimtafuta Mobeto ambapo simu yake iliita bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe kupitia mtandao wa WhatsApp, juu ya maneno anayosema Tunda, aliishia kusoma bila kujibu.
Hii si mara ya kwanza kwa wawili hawa kuingia kwenye bifu.
Awali walidaiwa kurushiana maneno ya chinichini, safari hii Tunda ameamua kumtolea uvivu ‘live’.
Post A Comment: