MBUNGE wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ ambaye ameachiwa huru leo Mei 10, 2018 kutoka katika Gereza la Ruanda jijini Mbeya alikokuwa amefungwa na Katibu wa CHADEMA Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga, amefunguka na kuweka wazi kilichojiri.
Amesema hakuwa anafahamu iwapo angeachiwa huru leo hadi polisi walipomfuata na kumwambia ajiandae. Amedai mapaka sasa hafahamu imekuwaje hadi akaachiwa kwani ilijulikana ataachiwa Juni 5, ambapo kifungo chake kingekamilika.
“Watu wote walitarajia ningetoka jela mwezi Juni, lakini ghafla jana niliambiwa nijiandae kwamba kesho asubuhi (leo) natakiwa niachiwe huru, nilipotoka nje nikakuta askari wengi, nikaelekezwa kuingia kwenye gari la RCO mimi na mwenzangu Masonga, tukasindikizwa na maofisa magereza watano hadi nyumbani na kutukabidhi kwa familia.
“Watu wanauliza, imekuwaje? Lakini mimi ninawaambia sijui, kwa sababu haikuwa kazi yangu kufanya hesabu za magereza, hiyo ni kazi ya magereza, kwa sababu mimi ninachoamini sikutakiwa kuwa magereza in the first place, utumishi uko palepale kwa level ileile, tulikuwa na exposure sasa hivi tumeongeza experience,” amesema Sugu.
Kuachiwa kwa watu hao ni jambo ambalo limewashtua wengi kwani inaaminiwa muda wake ulikuwa bado haujaisha.
Sugu na Masonga walitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miezi mitano jela Februari 26 mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya kwa kutoa lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli kwenye mkutano wa hadhara walioufanya Desemba 30 mwaka jana eneo la Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya.
Wameshatumikia adhabu hiyo kwa siku 73 ikiwa ni zaidi ya robo ya kifungo chao.
Post A Comment: