KAMPUNI ya Star Media (T) Ltd yenye chapa ya StarTimes imetangaza rasmi kurusha matangazo ya Kombe la Dunia Urusi mwaka 2018 Mubashara kupitia king’amuzi chake.
StarTimes imethibitisha kuonesha michuano hiyo jana katika hafla fupi iliyofanyika Terrace, Slipway Masaki jijini Dar es Salaam na kushirikisha waandishi wa Habari pamoja na wadau mbalimbali wa soka nchini.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Meneja Masoko wa Kampuni hiyo David Malisa alisema “Mwaka huu katika Kombe la Dunia la 21, StarTimes ni mrushaji rasmi wa michuano hiyo itakayoanza Juni 14 hadi Julai 15 nchini Urusi. Mechi zote 64 zitakazochezwa Urusi katika Kombe la Dunia zitarushwa moja kwa moja.
” Amefafanua mbali na kurusha tu michuano hiyo maarufu zaidi Duniani, StarTimes watarusha matangazo ya michezo yote katika lugha ya Kiswahili na hiyo ni katika jitihada za kuienzi na kuikuza lugha ya Kiswahili lugha ambayo ni maarufu zaidi katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.
“StarTimes tutarusha matangazo ya Kombe la Dunia, mechi zote 64 katika lugha ya Kiswahili pamoja na uchambuzi utakaoambatana na mechi hizo, uchambuzi utakaofanywa na wachambuzi mahiri na tuliowazoea hapa nchini”, ameongeza David.
Sambamba na kuzindua Kombe la Dunia, StarTimes pia wametangaza ofa kwa wapenzi wa soka, ambapo wateja watakaonunua king’amuzi au Luninga zao za kidigitali kati sasa na Juni 30 watapatiwa kifurushi cha juu hadi Julai 31 mwaka huu bure.
Post A Comment: