Kampuni ya SportPesa Limited leo siku Alhamisi tarehe 24 Mei imekabidhi hundi ya Shilingi Milioni 100 kwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, timu ya Simba SC.
Nahodha wa klabu ya Simba, Raphael Bocco (mwenye jezi nyekundu) akikabidhiwa mfano wa hundi ya Mil. 100 na viongozi kutoka SportPesa.
Hafla hiyo ya makabidhiano iliyofanyika kwenye ofisi za SportPesa ambao ni wadhamini wakuu wa Wekundu hao wa msimbazi zilizopo maeneo ya Masaki jijini Dar es Salaam, ilihudhuriwa na viongozi wa pande zote mbili kutoka SportPesa ni Mkurugenzi Mtendaji Ndugu Pavel Slavkov, Mkurugenzi wa Utawala na Utekelezaji Tarimba Abbas na Mkuu wa kitengo cha Operesheni, Luca Neghesti kutoka Simba ni Kaimu Makamu wa Raisi Ndugu Iddi Kajuna, Katibu Mkuu Hamisi Kissiwa , Msemaji mkuu wa kampuni Haji Manara pamoja na Mjumbe wa kamati ya Usajili Said Tulliy sambamba na wachezaji wote wa kikosi cha Simba wakiongozwa na nahodha John Bocco.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti wa SportPesa Ndugu Tarimba Abbas alianza kwa kuwapongeza wachezaji na viongozi wa Simba kwa kutwaa ubingwa.
Awali ya yote nianze kwa kuwapongeza viongozi na wachezaji wa Simba SC kwani mmewapa heshima kubwa wana msimbazi kote nchini na kubwa zaidi ni heshima mliyotupa sisi kama wadhamini wenu wakuu.” ndugu Abbas aliendelea kwa kufafanua kuhusu kiasi hicho cha pesa ambacho SportPesa imekabidhi kwa Simba kwa kusema;
Simba imeitendea haki nembo yetu ya SportPesa na kampuni inaamini kuwa kwa SportPesa kuwa wadhamini wakuu imekuwa ni moja ya chachu iliyosababisha Simba Sports Club kuchukua ubingwa huu. Tunachokifanya leo ni kutimiza moja ya ahadi tuliyotoa wakati tunasaini mkataba mwezi Mei mwaka jana kuwa tutatoa bonasi ya Shilingi Milioni 100 endapo mojawapo ya timu tunazozidhamini itachukua ubingwa wa Ligi Kuu, hivyo bila shaka timu ni Simba SC.”amesema Tarimba.
Naye Msemaji wa klabu ya Simba, Haji Manara ameipongeza Sportpesa kwa kuharakisha kutoa fedha hiyo mapema hata kabla ya Ligi kumalizika.
Manara amesema kuwa kwa sasa kilichobaki mbele yao ni kombe la SportPesa (SportPesa Super Cup) litakalofanyika nchini Kenya na ameahidi kuwa mwaka huu ni lazima klabu yake itachukua kombe hilo na kwenda Mjini Liverpool, Uingereza kuvaana na klabu ya Everton.
Ikumbukwe kuwa Simba SC ni miongoni mwa timu nne kutoka Tanzania zitakazoshiriki kwenye michuano ya SportPesa Super Cup itakayofanyika nchini Kenya kuanza Juni 3-10 ikishirikisha timu nane kutoka nchi za Tanzania na Kenya.
Timu nyingine ni pamoja na Yanga, Singinda United na JKU kutoka Tanzania sambamba na Gor Mahia, AFC Leopards, Kakamega Home Boys sambamba na Kariobangi Sharks kutoka Kenya ambapo mbali na kujizolea kitita cha Dola 30,000, bingwa wa michuano hiyo ataenda nchini Uingereza kucheza dhidi ya Everton FC kwenye dimba la Goodison Park.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: