KWA takwimu zilivyo ni kama Simba ikishinda mechi ya leo Jumapili dhidi ya Ndanda ambayo haijawahi kuwababaisha kwenye Uwanja wa Taifa, itakuwa imesaliwa na pointi mbili tu kutwaa ubingwa kabla hata Ligi Kuu Bara haijamalizika. 

Ambazo pointi hizo italazimika kuzifuata mjini Singida kwenye Uwanja wa Namfua dhidi ya wenyeji ambao tayar i wana uhakika wa kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho mwakani baada ya kufuzu fainali ya FA dhidi ya Mtibwa ambao wamefungiwa.

Lakini kwa lugha nyingine rahisi ni kwamba kama Simba akifanya yake leo na Yanga akapoteza mchezo wake na Mtibwa mjini Morogoro wiki ijayo, basi Mnyama tayari rasmi atakuwa mwakilishi wa nchi katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

 Simba ambayo kocha wao Pierre Lechantre ameomba kazi ya kuifundisha Cameroon, ikishinda mechi hiyo itakuwa imebakiwa na pointi mbili tu ambazo ikizipata itakuwa imemaliza kazi kwani Yanga hawatazifikia.

Yanga yenye pointi 48 ikishinda mechi zake zote zilizosalia kuanzia dhidi ya Mtibwa itamaliza msimu ikiwa na pointi 66 ambazo haziwezi kuisaidia endapo Simba atashinda japo mchezo mmojatu ujao.

Mpaka sasa Simba haijapoteza mchezo wowote tangu msimu huu uanze, Njombe Mji ikiweka rekodi ya kupoteza mechi nyingi zaidi ambazo ni 12 na Yanga ikiwa imepoteza michezo miwili.

 Simba imeweza kulinda heshima yake msimu huu kwani mastraika wake wawili ndiyo walioko kwenye nafasi mbili za juu kwenye msimamo wa wafungaji bora huku Yanga mshambuliaji wao mwenye mabao mengi akiwa ni Obrey Chirwa mwenye mabao 12.

Wachambuzi wa mambo wanasema sare ya bao 1-1 ambayo Yanga iliipata mjini Mbeya na baadaye wakakubali kupigwa na Simba ndiyo vitu vilivyowatoa kwenye mstari. 

Katika Ligi kubwa duniani, Barcelona ndiyo klabu pekee ambayo haijapoteza katika mechi zake 34 ilizocheza kwenye La Liga ambapo leo itakipiga na Madrid kwenye El Classico (Soma zaidi toleo maalum ndani).

Man City, PSG ndizo zimepoteza michezo miwili msimu huu kama Yanga ambayo nafasi yake ya kupanda ndege mwakani ni finyu. Katika hilo, Kocha Pierre anasema: “Tunatambua kila mchezo wetu ulio mbele kwa sasa ni mgumu. Tunajitahidi kupambana kuona kwamba tunapata matokeo bora zaidi. “Mchezo huu ni miongoni mwa mechi ambazo zitatupa nafasi ya sisi kutwaa ubingwa.” Mshambuliaji kiwembe wa Ndanda, Nassor Kapama amesema: “Mechi kiukweli itakuwa ngumu.”
Share To:

msumbanews

Post A Comment: