Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia elimu Mhe.Tixon Nzunda akizungumza na Makatibu Tawa!la Wasaidizi wa Mipango na Uratibu na Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kwenye kikao kazi cha kujadili tathmini ya uandaaji wa mipango na bajeti katika mwaka wa fedha 2018/2019 na miradi ya kimkakati kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa OR-TAMISEMI jijini Dodoma leo.
Mkurugenzi wa Tawala za Mikoa Beatrice Kimoleta akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia elimu Mhe.Tixon Nzunda kufungua kikao kazi cha kujadili tathmini ya uandaaji wa mipango na bajeti katika mwaka wa fedha 2018/2019 na miradi ya kimkakati kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa OR-TAMISEMI jijini Dodoma leo.
Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mipango na Uratibu na Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu Elimu ( hayupo pichani ) wakati akifungua kikao kazi cha kujadili tathmini ya uandaaji wa mipango na bajeti katika mwaka wa fedha 2018/2019 na miradi ya kimkakati kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa OR-TAMISEMI jijini Dodoma leo.
............................................................
Na Angela Msimbira, OR Tamisemi.
OFISI ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imetoa maelekezo ya kimkakati kwa Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mipango na Uratibu pamoja na Makatibu Tawala Wasaidizi wa Serikali za Mitaa kote nchini kuhakikisha wanakuwa chachu ya mabadiliko yenye kujenga ustawi wa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI anayeshughulikia elimu Mhe. Tixon Nzunda katika Kikao kazi cha kujadili tathmini ya uandaaji wa mipango na bajeti katika mwaka wa fedha 2018/2019 na miradi ya kimkakati kwa Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mipango na Uratibu na Makatibu Tawala wa Serikali za Mitaa kilichofanyika leo jijini Dodoma.
Akifungua kikao hicho Nzunda amesema kuwa ili kuleta mabadiliko yenye lengo la kujenga ustawi wa wananchi lazima kuwe na rasilimali watu wanaoamini mabadiliko, hivyo Makatibu Tawala Wasidizi wa Mipango na Uratibu na Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ndio viongozi wanaopaswa kuelimisha jamii kuhusu dira, dhima na programu ambazo Serikali inataka kufikia katika malengo makuu ya kujenga Ustawi wa wananchi.
Amewataka kubadilika kwa fikra, mtizamo, mwelekeo na mikakati ili kuleta mabadiliko makubwa katika uendeshaji wa Serikali kwa kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa na serikali katika kutoa huduma bora kwa jamii na kuleta maendeleo nchini.
“Ninyi ndio “engine” (gurumudu) ya kuleta maadiliko. Ndio kitovu cha kuleta Mabadiliko saidianeni na Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi, msiogope kuwashauri, kuwakosoa, na kuwaelekeza ili kuleta maendeleo katika jamii mnazozihudumia” Amesema Nzunda
Mhe. Nzunda amesema kuwa Serikali imejipanga kuona mabadiliko makubwa ya kiutendaji kuanzia ngazi za Serikali za Mitaa hivyo amewataka kutoa maelekezo ya Serikali yanazingatia Sera, sheria, kanuni na programu za uendeshaji kazi ndani ya Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
“ Makatibu Tawala wa Mipango na Uratibu na Makatibu Tawala Wasidizi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wanapaswa kujua dira ya Serikali na mipango ya Mikoa na kuwa na dhana ya usimamiaji na ufuatiliaji mtakuwa mmesaidia kuleta mabadiliko makubwa kwenye Mikoa yenu” Amesema Nzunda
Katika suala ya matumizi wa fedha za miradi Mhe Nzunda amesema kuna tatizo linaloendelea la kubadilisha matumizi ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi, fedha kukaa muda mrefu kwenye akaunti bila kufanyiwa kazi kwa malengo yaliyokusudiwa pamoja na kuchelewa kukamilika kwa miradi.
Aidha amezitaja baadhi ya changamoto za uandaaji wa mpango zinazoikumba mamlaka ya serikali za mitaa kuwa ni kutozingatia mpango mkakati, kutozingatia vipaumbele vya serikali pamoja na kushindwa kusimamia bajeti ipasavyo.
Katika hatua nyingine Nzunda ameoneshwa kukerwa na tabia za baadhi ya Wakurugenzi ambao hadi sasa hawajawalipa fedha za uhamisho walimu waliohamishwa kutoka shule za msingi kwenda kufundisha shule za sekondari wakati serikali ilishatoa fedha hizo, hivyo aliwataka suala hilo kusimamiwa kikamilifu.
Akizungumzia juu ya baadhi ya halmashauri kupata hati chafu na nyingine kutapa hati zisizoridhisha amesema kitendo hicho kinasababishwa na uzembe wa watu wengi na sio Mkurugenzi peke yake bali wahusika wote watawajibishwa ili kuhakikisha kuwa kila mtu anawajibika ipasavyo katika majukumu yake.
Awali akimkaribisha Naibu katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu, Mkurugenzi wa Tawala za Mikoa Bi. Beatrice Kimoleta amesema lengo la kikao hicho ni kujitathmini juu ya bajeti iliyomalizika sasa pamoja na kuandaa mipango na bajeti katika mwaka wa fedha 2018/2019.
Post A Comment: