Rais Dkt. John Pombe Magufuli amewataka wananchi wa Tanzania kiujumla kutovunja nyumba zao zilizoweka alama X yenye rangi ya kijanibila ya kupatiwa fedha zao za fidia kama inavyopaswa kwa mujibu wa sheria zilizowekwa.

Dkt. Magufuli ametoa kauli hiyo leo Mei 05, 2018 wakati alipokuwa anazungumza na wananchi wa Kijiji cha Mangula Mkoani Morogoro pindi waliposimamisha msafara wake na kutoa kero zao mbalimbali zinazowakabili katika maeneo yao

"Barabara hii tutaipanua, ila nashukuru Mungu nyumba nyingi hazipo kando kando ya barabara lakini nataka niwatolee ufafanuzi. Kwa mujibu wa sheria upande wa barabara ni mita 22.5 kila upande, mwaka 2007 pakafanywa mabadiliko kwenye barabara kuu na zile za mikoa kufikia mita 30, mabadiliko ya sheria hayo yalipokuwa yakiwekwa kuna baadhi ya nyumba zilikuwa zipo nje ya mita 22.5 kwa hiyo sheria ikawa imewakuta", amesema Rais Magufuli na kuongeza;

"Kuna nyumba zimewekwa alama ya X ya kijani, msibomee. Nyumba yako yenye X ya kijani hutakiwi kubomoa, siku utakayobomoa lazima uwe umepewa hela. Nataka muwaelimishe watanzania wote kuwa ukikuta nyumba yako au ukuta wako umewekwa alama ya X ya kijani na kijani wote mnaifahamu kama kuna mtu hajui rangi ya kijani aende angalie hata nguo za kijani za CCM".

Pamoja na hayo, Rais Magufuli ameendelea kwa kusema "Ukikuta X ya kijani maana yake wewe huna kosa ila hutakiwi kujenga nyumba nyingine katika eneo hilo na ukijenga nyumba nyingine utakuwa umefanya kosa kwasababu sheria imeshapitishwa tangu mwaka 2007. Lakini nyumba yako kama ilikuwepo na ikapigwa X maana yake barabara ikitaka kuja huko lazima ikupe mchuzi".

Kwa upande mwingine, Rais Magufuli amesema atasimama pamoja na wananchi wa watanzania katika kuwapambania masuala ya maendeleo
Share To:

msumbanews

Post A Comment: