Rais John Magufuli ameuagiza uongozi wa Manispaa ya Morogoro, kuweka utaratibu mzuri ili wamachinga waweze kuuza bidhaa zao ndani ya stendi ya mabasi ya Msamvu ya mjini Morogoro.
Kiongozi mkuu huyo wa nchi ametoa kauli hiyo jana Jumapili Mei 6, 2018 katika uzinduzi wa stendi hiyo, kubainisha kuwa yeye ni Rais wa Watanzania wote.
“Nimekuja kufungua stendi lakini si kufungua stendi ambayo ina ubaguzi. Nimechaguliwa na Watanzania wote. Niwaombe tu mtengeneze mkakati mpya kuwawezesha wamachinga kuruhusiwa kuingia humu na wapewe vitambulisho,” amesema.
Ametoa kauli hiyo baada ya kuuliza iwapo wamachinga wanaruhusiwa kufanya biashara katika stendi hiyo, kujibiwa na mamia ya waliofika kushuhudia uzinduzi huo.
“Fedha isiyojali maskini ni fedha haramu. Wito kwa waziri wa Tamisemi lazima kuwe na eneo la kufanya biashara kwa wamachinga wote katika stendi zitakazojengwa. Fedha zimnufaishe kila mmoja,” ameagiza Rais Magufuli na kuongeza:
“Mnawanyima nafasi wananchi wa hapa maana hawatauza mihogo, machungwa na bidhaa zao kwa wasafiri wanaopita hapa. Ninawaomba manispaa kuangalia jambo hili… lazima tutengeneze utaratibu mzuri utakaowanufaisha watu wote.”
Post A Comment: