KUUAWA kwa mdogo wake Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, John Heche Suguta , marehemu Suguta Chacha Suguta (27), mkazi wa Sirari kwa kuchomwa kisu mgongoni na askari Polisi wa Kituo cha Sirari, William Marwa mwenye cheo cha koplo na namba zake za kazi E.1156, kumeifanya familia ya marehemu kuikomalia Polisi.
Familia na ukoo wa marehemu huyo, bado inaendelea na vikao vya ndani chini ya Chacha Heche Suguta mdogo wake Mbunge Heche ambaye pia ni katibu wa Chadema Mkoa wa Mara.
Kikao hicho kilitoa azimio la kulitaka jeshi hilo la Polisi chini ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kanda ya Rorya/ Tarime, ACP Henry Mwaibambe lishiriki msiba huo kikamilifu kutokana na askari wao kutenda unyama huo. Familia pia ‘imekomaa’ kwa kulitaka jeshi hilo kuwafidia au kutoa mkono wa pole kwa wazazi wa marehemu kwa sababu walimtegemea kabla ya kufikwa na mauti hayo.
Marehemu Suguta Chacha Suguta
Chacha alisema kuwa marehemu anatarajiwa kuzikwa Kijiji cha Nyabitocho, Kata ya Mbogi wilayani Tarime, Mkoa wa Mara kama hakutakuwa na mabadiliko. ”Bado tunaendesha vikao vya ndani na juu ya ratiba ya mazishi ya marehemu mdogo wetu, ikikamilika tutaitoa” alisema Chacha.
Kiongozi huyo alitumia nafasi hiyo kufafanua kuwa aliyefariki ni mdogo wake sio yeye kama ilivyoenea katika mitandao mbalimbali ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari ambavyo viliweka picha yake na kuchapwa jina lake. ”Napenda kuwafahamisha kuwa aliyeuawa ni mdogo wangu Suguta sio mimi, ninaomba Watanzania wenye mapenzi mazuri wanaotufariji niwafahamishe hivyo,”alisema Chacha.
Aliendelea kusema kuwa tayari wageni mbalimbali wanaendelea kufika msibani hapo na kusaini kitabu cha rambirambi ikiwa ni pamoja na Mbunge wa Viti Maalum wa Serengeti (Chadema), Catheline Nyakao Ruge.
Post A Comment: