Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,  Dk Mwigulu Nchemba amewataka wasioridhishwa na utendaji kazi wa Jeshi la Polisi kukata rufaa kwake.

Pia, amewataka wanasiasa wanaozungumzia matukio ya kupotea watu kuwa na ushahidi wa kutosha na kama hawana wasiyazungumze kwani yanajenga taswira hasi kwa nchi.

Ametoa kauli hiyo wakati akijibu hoja za wabunge walizozitoa katika mjadala wa bajeti ya wizara hiyo mwaka 2018/19 na kubainisha kuwa si askari wote ni wema na kwamba  wanaokiuka taratibu za kazi hatua zitachukuliwa dhidi yao.

“Damu ya mwanadamu haiwezi kulinganishwa na thamani ya chama chochote au kabila lolote na sisi hatutakubali damu imwagike bure lakini  panapotokea tatizo la kiutendaji la aina hiyo, hilo ni la mtu mmoja,” amesema.

Kuhusu watu wanaopotea amesema, “Kuna mambo mengi ya kimaadili tumeyafanyia msako, kuna watu wamehama majumbani mwao  kwa msako wa dawa za kulevya na wengine tumeambiwa wamevuka mipaka ya nchi yao na ndio hao wanasema wamepotea na ukituuliza yuko wapi na sisi tutasema yupo wapi.”

Amesema kuna ambao wamekimbia baada ya baadhi ya watu waliokamatwa kuwataja kuwa wanatumia silaha.

“Ukijumlisha hao ambao hawapo na kusema wamekufa hiyo siyo sawa kwani kwa sasa Watanzania ambao wanashikiliwa nje ya nchi katika magereza ni zaidi ya 1,000. Ukisema hao watu wameuawa ni makosa,” amesema.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: