Mwanasheria wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Gwakisa Mlawa, amedai mahakamani kwamba Bodi ya Wakurugenzi ya shirika hilo haikujua chochote kuhusu mkataba ulioingiwa kati ya aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu, Tido Mhando na Channel 2 Group Corporation (BV1).

Mlawa alidai pia mshtakiwa anayekabiliwa na tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh. milioni 887.1, aliingia mkataba huo bila baraka za bodi ya zabuni ya TBC.

Shahidi huyo wa pili alitoa ushahidi wake jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Leonard Swai, shahidi huyo alidai kuwa hakuwahi kuufahamu mkataba huo hadi alipopokea taarifa za kesi Juni, 2012 kutoka Channel 2 Group Corporation (BV1) kwamba TBC imekiuka mkataba wa kuwekeza mitambo ya digitali.

"Mheshimiwa hakimu mkataba huo ulisainiwa kati ya Tido na watu wawili wa Channel 2 Group Corporation (BV1). Pia kulikuwapo na nyongeza ya mkataba uliotiwa saini kati ya Juni, Agosti na Novemba mwaka 2008... TBC tulimwandikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kuomba ushauri naye aliagiza ateuliwe mwanasheria wa kimataifa ambaye ni mjuzi katika masuala hayo," alidai shahidi na kuongeza kuwa:

"Iliteuliwa kampuni ya uwakili ya Freshfield Bruckhaus Derringer us LLP ilikuja nchini TBC kufanya uchunguzi wa nyaraka na kwamba ililipwa malipo ya awali zaidi ya Sh. milioni 800...katika uchunguzi huo, ulibaini kuwa Tido alisababisha hasara ya fedha hiyo iliyokuwa kampuni ya uwakili," alidai Mlawa.

Alipohojiwa na wakili wa utetezi, Ramadhan Maleta, kama aliiona mikataba hiyo, shahidi alidai kuwa ilikuwa kama wameingia makubaliano ya awali ya maandalizi ya mchakato wa kuelekea kwenye digitali.

Katika kesi ya msingi, inadaiwa kuwa Juni 16, 2008, akiwa Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Tido ambaye alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC, kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa kutia saini mkataba wa kuendesha na utangazaji wa vipindi vya televisheni kati ya TBC na channel 2 Group Corporation (BV1) bila kupitisha zabuni, kitu ambacho ni kinyume na Sheria ya Ununuzi na kuinufaisha BVl.

Katika shtaka la pili, Tido anadaiwa kutumia vibaya madaraka yake Juni 20, 2008 alipotia saini makubaliano kwa utangazaji wa digitali duniani kati ya TBC na BVl.

Katika shtaka la tatu, anadaiwa Agosti 11, 2008 na Septemba 2008 akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kutia saini mkataba wa makubaliano kwa ununuzi, usambazaji kufunga vifaa vya usambazaji na mnara wa utangazaji kati ya TBC na BVI na kuifaidisha BVI.

Katika shtaka la nne, anadaiwa kuwa Novemba 16, 2008 akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kutia saini mkataba wa makubaliano kwa kuendesha miundombinu ya utangazaji (DTT Broadcast Infrastructure) kati ya TBC na BVI na kuinufaisha BVI.

Katika shtaka la mwisho, anadaiwa kuwa kati ya Juni 16 na Novemba 16, 2008 akiwa UAE, Tido aliisababishia TBC hasara ya Sh. 887,122,219.19.

Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa leo ushahidi wa Jamhuri.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: