Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Janeth Masaburi amemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Mwigulu Nchemba kutoa taarifa bungeni juu ya vifo vya wanasiasa Chacha Wangwe aliyekuwa Mwenyekiti wa chama cha DP, Mchungaji Christopher Mtikila.
Wangwe ambaye alikuwa mbunge wa Tarime kwa tiketi ya Chadema alifariki dunia Julai 27 mwaka 2008 katika ajali ya gari iliyotokea Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, Mtikila alifariki katika ajali ya gari Oktoba 4, 2015 Chalinze wilayani Bagamoyo.
Akichangia bajeti ya wizara hiyo mwaka 2018/19, Masaburi amemtaka pia waziri huyo kutoa taarifa za kifo cha watalii waliomwagiwa tindikali na makanisa yaliyochomwa moto.
“Tunaomba taarifa, kifo cha Wangwe, Mtikila, watalii waliomwagiwa tindikali na makanisa yaliyochomwa moto Zanzibar,” amesema.
Kuhusu amani amesema Tanzania ipo mahali salama tangu kuasisiwa kwake enzi ya Hayati Mwalimu Nyerere na maraisi wastaafu Ali HassaMwinyi, Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete.
“Hii nchi yetu sote, humu tupo zaidi ya 300 ila Watanzania wapo milioni 60, kila mtu ana haki hamasa ambazo zinatolewa kwa kutubagua zishindwe kwa jina la yesu. Bila amani hatuwezi kulima hakuna kwenda shule, kustarehe wala kuzaliana,” amesema.
Amesema watu wasitanie amani kwa kutumia dini kwamba dini fulani inaonewa na kuhoji mbona wapo ndani ya Bunge.
“Tusitanie amani, ninaomba Serikali iongeze bajeti ya kutosha katika vyombo vya ulinzi na usalama pia makazi yao yaboreshwe na kujengwa nchi nzima,”amesema.
Post A Comment: