Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Taifa (CHADEMA) Mhe, Freeman Mbowe amefunguka na kutoa neno kuhusu madiwani 46 ambao wamejiuzulu nafasi zao na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kusema kuwa jambo hilo linafanywa na CCM kwa lengo la kuwakatisha tamaa wana CHADEMA.
Mbowe amesema kuwa wapo watu wanadhani kitendo cha baadhi ya madiwani kuhama CHADEMA na kwenda CCM ni kukiuwa chama hicho na kusema suala hilo haliwezi kutokea kwani madiwani wa CHADEMA nchi nzima wapo zaidi ya 1130 huku madiwani 46 ndiyo waliohama na kwenda CCM na kusema kitendo hicho kinawapa funzo katika maandalizi ya kutafuta viongozi ambao kweli wanaweza kukisimamia chama na si wale wanaotafuta fursa za kutoka kupitia uongozi.
"Kazi kubwa inayofanywa na CCM ni kuwakatisha tamaa na jambo ambalo limefanyika karibuni ambalo linaonekana wana CHADEMA wengi wamerudishwa nyuma basi ni suala la madiwani.
"Madiwani wamenunuliwa jamanii wanaunga mkono juhudi, kuna watu wengine ni mizigo lakini sasa tunafanyaje lakini watu wa CHADEMA wanakata tamaa eti madiwani wanaisha chama kinakufa
"Hiki chama hakifi mzee CHADEMA nchi nzima ina madiwani 1184 madiwani mpaka dakika hii wameondoka ni madiwani 46 kwa hiyo tuna madiwani zaidi ya 1130 wamebaki CHADEMA halafu mtu anasema CHADEMA inakufa una akili wewe?"
Aidha Mbowe amesema kuwa hao viongozi ambao wanahama kutoka CHADEMA na kwenda CCM kwao ni kama funzo kwamba wapo viongozi na watu mbalimbali ambao wapo ndani ya CHADEMA kwa lengo la kutafuta fursa tu na wanapoikosa hiyo fursa na ulaji wanaamua kuondoka.
"Kwetu ni funzo tunapojiandaa kwenda kwenye uchaguzi wa Wenyeviti wa Mtaa, Vijiji, madiwani, wabunge hata nafasi ya Urais tukajiandaa na kina nani wanaoishi ndoto ya CHADEMA lazima safari hii tujiridhishe mapema huyu tukimpa nafasi basi historia yake tunaijua vyema" alisema Mbowe
Post A Comment: